Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mlima Kilimanjaro ndio chanzo cha Raia Wa Ethiopia Kutengenezewa Hati za Kusafiria

Mlima Kilimanjaro, ambao hifadhi inayoizunguka, inatimiza miaka 50 mwaka huu, ndio chanzo cha raia wa Ethiopia kutenenezewa pasi zao za kwanza kabisa za kusafiria.

Aliyekuwa mkuu wa kwanza wa majeshi nchini Tanzania, Jenerali Mirisho Sarakikya, anabainisha.

Sarakikya anasimulia kuwa yeye ndiye aliihawishi serikali ya Ethiopia kuanza kutoa hati za kusafiria kwa raia wake, ili kuwawezesha kuja nchini, kwa ajili ya kuupanda Mlima Kilimanjaro.

Jenerali Sarakikya anafafanua kuwa awali serikali ya Ethiopia haikuwa ikitoa ‘passports,’ kwa raia wake, ikihofia kuwa iwapo watasafiri nje ya nchi hiyo, basi wanaweza kulowea ughaibuni moja kwa moja.

Hata hivyo kipindi chake kama Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, enzi za utawala wa Mengistu Haile Mariam, Sarakikya alikuwa anatumia muda mwingi kutangaza utalii wa Tanzania lakini hasa Mlima Kilimanjaro.

Jenerali Sarakikya alikuwa Balozi nchini Ethiopia kwa kipindi cha miaka kumi kati ya mwaka 1984 hadi 1993.

Jenerali Sarakikya enzi zake

Hata wa rais wa Mpito Tesfaye Gebre Kidan Geletu alimkuta na kumuacha, na vile vile alihudumu kipindi cha Meles Zenawi Asres.

Awali Jenerali Sarakikya alikuwa akiiwakilisha Tanzania nchini Nigeria kuanzia mwaka 1977 hadi 1984.

Kote huko alikuwa akiutangaza Mlima Kilimanjaro, ila sasa kwa upande wa Ethiopia ilibidi atumie nguvu zaidi maana serikali haikutaka watu wake wasafiri nje ya nchi hiyo.

Na juhudi zake za kuwashawishi wakazi wa nchi hiyo kuja kuutembelea mlima huo mrefu zaidi barani Afrika, hatimaye zilizaa matunda.

Waethiopia wengi walionesha kuvutiwa na wazo la kupanda Kilimanjaro.

Sasa tatizo lilikuwa ni jinsi gani wao wangeweza kusafiri nje ya nchi, maana kipindi hicho, serikali yao ilikuwa haitoi passport kwa wananchi wake. Ikiwakataza kusafiri kutoka nje ya mipaka.

Lakini Jenerali Sarakikya aliandaa andiko maalum na kulipeleka kwa maofisa wa serikali ya Ethiopia, akiwemo waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo. kuwaombea raia wake ruhusa ya kusafiri hadi Tanzania kwa ajili tu ya kupanda Mlima Kilimanjaro, na sio vinginevyo.

Serikali ya Ethiopia hatimaye ilikubali wazo hilo la kuanza kutoa hati za kusafiria kwa raia wake ili waweze kupanda Mlima ulioko Tanzania.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sarakikya ilikuwa ni kwa masharti kwamba Tanzania ingebeba jukumu la kuhakikisha kuwa raia hao wa Ethiopia wanarudi kwao haraka, mara baada ya utalii huo wa kupanda mlima.

Jenerali Sarakikya alipowahakikishia kuwa Tanzania itawarejesha Waethiopia wote nchini kwao mara baada ya kushuka kutoka kileleni, serikali ikaanza kutoa pasi za kusafiria.

“Tunaweza kusema kuwa Mlima Kilimanjaro hasa ndio chanzo serikali ya Ethiopia kuanza kutengeneza pasi za kusafiria kwa wananchi wake,” alisema Jenerali Sarakikya katika mahojiano ya hivi karibuni.

Na baada ya waethiopia waliokuwa wanakuja Afrika Mashariki kupanda Mlima Kilimanjaro kurejea kwao salama. Serikali yao ikaanza kuchapisha pasi nyingine nyingi za kusafiria.

Na asilimia kubwa ya pasi hizo ndizo baadae sana ziliwawezesha waethiopia kuanza kusafiri sehemu nyingine nyingi duniani baada ya masharti kulegezwa.

Hadi leo kuna baadhi ya WaEthiopia ambao wamesambaa sehemu nyingi duniani wanaomkumbuka na hata kumpigia simu Jenerali Sarakikya wakimshukuru kwa kuanzisha kampeni ya kupanda mlima Kilimanjaro nchini kwao.

Na wengi wanajua kuwa utalii wa Mlima Kilimanjaro, nchini kwao ndio uliozalisha pasi za kwanza za kusafiria za Ethiopia.

Jenerali Sarakikya alikuwa balozi wa Tanzania katika nchi za Ethiopia, Nigeria na Kenya kwa nyakati tofauti.

Yeye pia ameweka historia ya kuwa Mtanzania aliyepanda Mlima Kilimanjaro mara nyingi zaidi.

Jenerali Sarakikya amefanikiwa kufika katika Kilele cha Uhuru kwa mara 41.

Mbali na Kilimanjaro, Sarakikya pia ameupanda Mlima Meru ambao ndio wa pili kwa urefu nchini, ulio ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha.