Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mashujaa Wasiofahamika: Askari wanaolinda Maliasili na Masahibu yanayowakuta wakiwa kazini

Iwe Usiku au Mchana Yeye hudamka alfajiri kufanya doria au wakati mwingine kulazimika kukesha usiku kucha lindoni.

Na doria yenyewe ni ile ya hatari; kukabiliana na majangili wa wanyamapori na misitu.

Licha ya kuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 10 lakini askari Richard Michael (38), mmoja wa walinzi 36 wa eneo la mapito ya wanyama (Ushoroba) wa Kwakuchinja lililopo mkoani Manyara, hawezi kamwe kusahau alivyonusuka kifo mikononi mwa kundi la wahalifu.

“Mwaka 2014 nilinusurika kuuawa mikononi mwa wafugaji 15 baada ya kunishushia kipigo kikali kilichonipelekea kuvunjika mkono wangu wa kushoto,” amesema Michael (Maiko).

Ushoroba wa Kwakuchinja uliopo katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara eneo la Makuyuni, imekuwa njia kuu ya wanyamapori kutoka hifadhi hizo mbili kusaka mahitaji yao muhimu kama chakula, maji na kuzaliana.

Maiko amesema kuwa anakumbuka siku ya tukio Jumanne Aprili mwaka 2014 akiwa doria na wenzake watatu msituni aliona ng’ombe wakiwa eneo la kitaluni ambalo haliruhusiwi kuchungwa mifugo.

Amesema kuwa katika kujaribu kusogelea mifugo hiyo ili kuwaondoa walijikuta mikononi mwa wafugaji  waliojificha kichakani wakiwa wamejiandaa kwa shari ambapo waliwashambulia kwa kipigo cha viboko na marungu.

“Baada ya kuzidiwa na mashambulizi wenzangu walifanikiwa kukimbia na kuniacha pekee yangu na bahati mbaya sikuwa na silaha yoyote zaidi ya fimbo nene ambayo nayo ilitumika kuniadhibu,” amesema na kuongeza;

“Kutokana na baadhi ya wafugaji hao nilikuwa nawafahamu nilijaribu kuwataja kwa majina wanionee huruma lakini haikusaidia kwani walizidi kunipiga hali iliyonisababishia maumivu makali ya mwili, kupoteza damu nyingi, lakini pia kuvunjwa mkono.”

Baada ya kuonekana na hali mbaya huku akivuja damu nyingi sehemu mbalimbali za mwili wake, amesema wafugaji hao walikimbia na mifugo yao na kumuacha hapo.

“Nililala hapo nikiwa sijitambui hadi askari wenzangu waliokuwa wamekimbilia kambini kuomba msaada wa kuongezewa nguvu walipofika na kunichukua kunipeleka hospitali ya Mrara iliyoko Magugu kwa matibabu,” amesema.

Michael amesema kuwa kutokana na hali aliyokuwa nayo wengi walimkatia tamaa ya kupona lakini baada ya matibabu ya miezi mitatu mfululizo sasa anaishi na anaendelea na kazi zake za ulinzi wa wanyamapori na misitu ndani ya eneo la Kwakuchinja chini ya taasisi ya Chem chem Association.

Simulizi ya Maiko haitofautiani sana na hadithi ya James Nyasuka aliyeachiwa alama ya matundu ya meno katika mkono wake wa kulia wakati akipambana na jangili aliyejaribu kumuua tembo katika eneo la Hifadhi ya Ziwa Manyara.

Amesema kuwa siku ya tukio akiwa doria walikumbana na majangili watatu ambao wengine walipowaona askari walikimbia lakini mmoja waliofanikiwa kumkamata wakati anapambana nae akijihami asichomwe na kisu alichokuwa ameshika huyo. Katika purukushani hizo, askari huyo alijeruhiwa vibaya kwa kung’atwa.

“Wenzangu waliendelea kuwakimbiza wengine na mimi nikamkamata huyu aliyekuwa ameshika kisu na kwa sababu sikuwa na silaha yoyote tulipigana kwa mikono na baada ya kuona namzidi nguvu alining’ata na meno mkono wangu lakini nashukuru Mungu nilimkamata na sheria ikachukua mkondo wake na mimi leo nimepona,” amefafanua James.

Mbali na majeraha, amesema ziko hatari nyingi walizokumbana nazo ikiwemo kukoswakoswa mishale na mikuki wakiwa doria kuzuia majangili lakini pia wafugaji wasiingize mifugo ndani ya hifadhi.

“Kiukweli katika kazi hii kuna hatari nyingi sana za kunusurika kuuawa katika kutetea ulinzi wa rasilimali zetu, lakini tunapambana hivyo hivyo kuhakikisha vizazi vijavyo wanakuja kufaidi tunu hii ya Taifa,” amesema James.

Walinzi wa Maliasili: Gari la Askari wa wanyamapori likiwa limekwama porini. Majukumu ya watu hawa sio tu kwamba ni magumu bali pia ni hatari (Picha na Bertha Mollel)

Ukiachana na kujeruhiwa mwili na kusababishiwa ulemavu,  wapo askari wa uhifadhi ambao walipoteza mali kutokana na kulinda maliasili kama ilivyomtokea Lucas Mollel aliyepo katika eneo hilo hilo la Kwakuchinja.

Lucas amesema kuwa kutokana na kulinda rasilimali miti isivunwe kiholela na kuchomwa mkaa ndani ya Tarangire amejikuta akiwekewa kisasi hadi kusababisha familia yake kunusurika kuuawa baada ya watu wasiojulikana kuchoma nyumba yake usiku wa manane.

“Ni matukio ya kutisha maana kuna wenzetu hata tumeshuhudia wakipoteza maisha wakati wakitekeleza majukumu yao au kulipiziwa visasi lakini tunaendelea kupambana kwa ajili ya maisha ya familia zetu wapate mahitaji yao lakini pia uendelevu wa rasilimali hizi,” amesema Lucas.

Simulizi hizo ni sehemu ndogo tu ya madhila wanayokumbana nao askari na maofisa wa uhifadhi nchini.

Tarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyowasilishwa Bungeni Dodoma wakati wa bunge la Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 inaonesha kuwa askari na maafisa wa jeshi la uhifadhi 21 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa katika vipindi tofauti msimu wa mwaka 2022/2023 wakati wakitekeleza majukumu yao ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za wanyama pori na misitu.

Maofisa hao ni wale waliojitoa kuishi misituni na maporini kulinda rasilimali wanyama pori na misitu lakini wakauawa, na wahalifu.

Kwa mujibu wa Waziri Husika vitendo hivyo vinaumiza na kusikitisha.

“Serikali hatuna namna ya kuwalipa mashujaa hawa zaidi ya kuwaombea na kuwatambua pia kuwathamini daima milele lakini pia kuendeleza walipoishia katika kuzilinda rasilimali zetu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Ili kupunguza madhila hayo Serikali na wadau wengine wa uhifadhi wamekuwa wakiweka jitihada za kuwawezesha askari na vifaa vya kisasa na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda maliasili.

Kuna Jitihada zozote za kuwasaidia askari hao?

Meneja wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Chem Chem Association, Martin Mung’ong’o amesema katika kukabiliana na hatari hizo wanazokumbana nazo askari katika ushoroba wa Kwakuchinja wamejikita kutoa elimu kwa wananchi na wanafunzi juu ya umuhimu wa kuhifadhi maliasili na wanyamapori kwa ajili ya maendeleo ya ushoroba wa na utalii kwa ujumla.

Chem Chem ni moja ya wadau wanaoendesha miradi mbalimbali ya kuelimisha jamii kwa ajili ya kunusuru Kwakuchinja chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili ambapo wanalenga kuwafikia wanafunzi 400 kutoka shule mbalimbali watakaokuwa mabalozi viongozi shuleni.

“Kwa miaka hii mitatu 2022 hadi 2024 tunalenga kuwafundisha wanafunzi 400 ambao hadi sasa Desemba, 2023 tumeshawafikia wanafunzi 191 ambao tumewaingiza kwenye mradi wa elimu vijana kwa ajili ya kupunguza uhalifu wa uhifadhi,” amesema.

Vikwazo kutokomeza uhalifu hifadhini

Licha ya kutoa mafunzo, Mung’ong’o amesema changamoto kubwa katika kukabiliana na uhalifu wa hifadhini ni utaalamu finyu miongoni mwa maaskari juu ya namna ya kuanzisha mchakato wa kufungua kesi hadi kuwasilisha ushahidi ili watuhumiwa watiwe hatiani.

Kwa kawaida, anasema uendeshaji wa kesi kuchukua muda mrefu na kusababisha mashahidi kukata tamaa au kushawishiwa kubadilisha udhahidi kwa vitisho au rushwa.

“Changamoto nyingine ni watuhumiwa wanaoharibu misitu au kuingiza mifugo hifadhini kupewa adhabu ndogo ya kutozwa  faini ya kiasi cha shilingi 50,000/- kitendo ambacho hakimalizi uhalifu,” amefafanua.

Uhifadhi shirikishi wapunguza matukio hayo

Mamlaka na wadau wa uhifadhi katika ushoroba wa Kwakuchinja wanaendesha miradi yenye manufaa kwa jamii inayohusiana na uhifadhi ili kuwasaidia wananchi kuona umuhimu wa kuhifadhi bioanuai. .

Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge, Benson Mwaise amesema kuwa jumla ya vijiji 10 vilivyoko ndani ya mapito ya wanyama ya Kwakuchinja wananufaika kwa kuvipatia zaidi ya milioni 100 kila mwaka kama mgawo wa faida wanayopata kutokana na shughuli za kitalii na uhifadhi.

Amesema lengo la kuvipatia vijiji fedha hizo ni kiwawezesha kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta ya afya, elimu, mazingira na ujasiriamali kupunguza tamaa ya kufanya uhalifu katika ushoroba huo.

Kutokana na mapato ya shughuli za kitalii, Burunge inaweza kugharamia shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na uoto wa asili katika eneo la mapito ya Wanyama ndani ya uwanda wa Tarangire-Manyara.

“Kwa minajili hiyo, wananchi hupata mwamko wa kushiriki katika masuala ya uhifadhi pamoja na vita dhidi ya ujangili badala ya kuuharibu,” amesema Mwaise.

Vile vile wanawake wa maeneo ya Hifadhi ya jamii ya Randilen sasa wanaweza kutengeneza bidhaa za mapambo kwa ajili ya kuwauzia watalii wa kigeni kupitia taasisi ya ‘Asilia Giving,’ kwa kushirikiana na Utafiti wa Simba Tarangire pia na USAID Tuhifadhi Maliasili.

Zakaria Israel, Afisa Mradi wa Shirika la Asilia Giving amesema wanawake wa maeneo hayo wamenufaika vilivyo na mradi huo na wengi wameweza kuwasomesha watoto na hata kujenga makazi jambo ambalo pia limepunguza jamii hiyo kutegemea rasilimali za wanayamapori na misitu kujiingizia kipato na kupunguza ujangili.

Mara nyingi serikali huwataka wananchi kutii sheria bila shuruti na pia kuwachukulia askari kama wazalendo waliojitolea katika katika ulinzi wa nchi.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili, Mohammed Mchengerwa aliwasihi watanzania kusaidia askari hao katika kutekeleza majukumu yao na sio kuwakwamisha.

Aliongeza kuwa ndani ya mwaka mmoja kati ya Aprili 2022  na Aprili 2023 Serikali iliwakamata watuhumiwa 12,058  kwa tuhuma mbalimbali za uhalifu wa uhifadhi ikiwemo ujangili, uvunaji mistu na kuvunja mitandao saba ya ujangili.

Askari wa hifadhi waliouawa kazini kipindi cha Mwaka 2022/2023

Hawa ni Baadhi tu ya askari wengi ambao wamekuwa wakipoteza maisha au kujeruhiwa vibaya wakati wakiwa katika majukumu ya kulinda maliasili 2022/23

Deus Mwakajegela alifariki kwa kuchomwa mkuki mwaka 2022 akilinda mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

James Karomba aliyeuawa na wafugaji katika Pori la Akiba Inyonga.

Mwita Msabi aliyeuawa na majangili akiwa doria katika hifadhi ya msitu Udzungwa.

Chanzo: Wizara ya Maliasili na Utalii