Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Ziwa Manyara na sakata la wavuvi dhidi ya mabadiliko ya Tabia ya Nchi

Majira ya saa tano asubuhi, pembezoni mwa Ziwa Manyara, wavuvi watatu wamekaa ndani ya maji mita chache kutoka kwenye fukwe wakivuta nyavu huku wakiwavuna samaki walionasa.

Samaki hao waliovuliwa, walikuwa wadogowadogo sana wasiozidi urefu wa sentimita 10 wakati wanaoruhusiwa kuvuliwa nchini ni sentimita 25 na kuendelea.

Katika ndoo tatu za lita 20, wavuvi hao waliokuwa wamevalia bukta na fulana  nyepesi zilizopoteza rangi zao halisi tena, walikuwa wamevuna samaki kidogo aina ya Tilapia na kambale mmoja kila ndoo.

Mmoja wa wavuvi hao Afia Mameda anaiambia ‘Taifa la Tanzania’ kuwa hali hiyo sio kawaida kulinganisha na miaka ya nyuma ambapo waliweza kutegemea shughuli hiyo pekee kukidhi mahitaji ya familia kutokana na wingi wa samaki waliokuwa wanapatikana kwenye ziwa hilo. 

Kwa sasa hali ni tofauti na samaki waliowapata ni wachache zaidi ya wale waliowategemea. 

Ziwa Manyara ambalo ni la saba kwa ukubwa hapa nchini likiwa na  kilomita za mraba 470 na kina cha mita 3.5 hadi nne, linapatikana katika mikoa miwili ya Arusha na Manyara, hususan wilayani Babati na Monduli.

Mvuvi akivuta jarife lenye samaki wadogo ziwani (Picha na Bertha Mollel)

 Afia anasema kuwa samaki hao waliokuwa wanapatikana hapo soko lake kubwa ni katika mahoteli yaliyo karibu na hifadhi ya Manyara, Babati mjini lakini wale wakubwa walisafirisha hadi jijini Arusha.

Afia analalamika kuwa ukame wa mara kwa mara umesababisha samaki kuwa wachache mno wasiokidhi hata soko la Magugu hivyo pia wao kushindwa kutimiza mahitaji ya familia kwa shughuli hiyo pekee.

“Msimu wa samaki hapa ni hadi kipindi cha Mvua ambayo ikinyesha maji hujaa ziwani na samaki huzaliana kwa wingi pia hukua haraka na hupatikana kwa wingi,” anaeleza Afia

Mvua zikizidi sana huwa hatari kidogo kwani maji hujaa ziwani hadi kuelekea kwenye mashamba ya watu ambapo Afia anasema kuwa husababisha wakazi wengi kuacha shughuli zao za kilimo na kuvamia shughuli hiyo ya uvuvi.

“Mvua zikizidi hapa kilimo kinashindikana matokeo yake watu wanakuja ziwani kila mmoja anataka kuvua samaki ndio vurugu inapotokea na wakati mwingine samaki kuvuliwa kwa kasi hadi kutishia kizazi chao,” anaeleza. 

Wavuvi wajawa na hofu

Ziwa hili ambalo huendeshwa shughuli zake kipindi cha mvua pekee, imeonekana kuleta hofu zaidi kwa wavuvi wa ziwa hilo kiasi cha kuiomba serikali kuona jinsi ya kulifanya liwe endelevu kuliko kuwa la msimu kama sasa.

“Pamoja na ziwa kuwa na maji mengi kipindi hiki ambacho mvua imenyesha kidogo, kuna wakati hukauka kabisa kutokana na ukame na kusababisha kufungwa na halmashauri na watu wa Burunge,” anasema mvuvi mwingine, Huseni Tamath. 

Kutokana na hilo, Huseni anaiomba serikali kufanya ziwa hilo kuwa endelevu lisikauke kwa kuangalia jinsi ya kuelekeza mikondo ya mito iliyopo nyanda za juu iweze kutiririsha maji Ziwa Manyara.

“Ziwa hili wengine ndio maisha yetu yanategemea hapa lakini Kuna kipindi linakauka kabisa na kina kidogo kinabaki hifadhini ambako haturuhusiwi kuvuna, hivyo serikali ituangalie na sisi kwa kuhakikisha halikauki,” amesema Husseni.

Kwa mujibu wa wavuvi hao ziwa likikauka msimu wa kiangazi baadhi ya watu huvamia na kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji hadi eneo la ziwani zinazohusisha upuliziwaji wa dawa za mimea na wanyama jambo ambalo ni hatari kwa viumbe vya majini.

Mfano, Afia ameeleza kuwa maji ya mvua yanapofika kwenye maeneo yaliyotumika kwa kilimo huzoa sumu zitokanazo na kemikali za viuatilifu zinazotumika na wakulima kuulia visumbufu mimea au mbolea za kustawisha mazao yao na kuyatupa ziwani.

Madhara ya Sumu za Kilimo zinavyoathiri viumbe hai ndani ya hifadhi ya ziwa Manyara 

 Ziwa Manyara mbali ya kuwa makazi ya viumbemaji kama samaki, lakini pia ni chanzo cha maji ya kunywa kwa viumbe hai wengine wanaopatikana katika hifadhi hiyo kama ndege na wanyamapori wakiwemo tembo, nyati, swala na wengineo wanaopatikana hifadhini.

Askari wa uhifadhi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge wanaolinda ziwa hilo upande wa ushoroba wa Kwakuchinja, Richard Levilal, anaeleza kuwa sumu hizo zitokanazo na shughuli za kilimo zimekuwa chanzo cha vifo vya samaki lakini pia ndege hasa aina ya korongo na flamingo wanapokunywa.

“Tulibaini chanzo hicho baada ya kuona tatizo na kufanya utafiti, hivyo kwa sasa kipindi cha ukame tunalinda watu wasilime eneo la ziwa,” anasema Levila na kuongeza..

“Hata hivyo tatizo limebaki mvua zikizidi na maji kujaa hadi kufuata maeneo ya mashamba ambayo sio eneo la ziwa, jambo ambalo hata hivyo halitokei mara kwa mara.”

Hatari kwa kizazi cha samaki

Mbali na sumu itokanayo na viuatilifu na mbolea inayotumia katika kilimo kuhatarisha kizazi cha samaki lakini pia mwenendo wa uvuvi usiozingatia kanuni na taratibu umeonekana hatari nyingine.

Aafeez Jivraj, mwekezaji katika sekta ya hoteli za kitalii katika ufukwe wa Ziwa Manyara, yeye anaonesha hofu yake ya siku moja ziwa kukosa samaki kabisa.

“Mwenendo wa uvuvi sio salama sana katika ziwa hili ndio maana Miaka ya hivi karibuni samaki wamepungua sana hasa Tilapia,” amesema Jivraji na kuongeza. 

“Tilapia jike huwa wanabeba mayai midomoni, lakini wavuvi huwavua hata wakigundua yuko na mayai hayo, kitendo ambacho ni hatari sana kwa kizazi cha samaki.”

Samaki mmoja hubeba mayai 100 mdomoni, hivyo endapo wakivuliwa kumi, Jivraj amesema ni upotevu wa zaidi ya vizazi 1000.

Mbali na hilo ameitaka Mamlaka za serikali kufanya utafiti upya wa kuiwekea ziwa hilo mipaka ili litambulike kwa ajili ya kuondoa migogoro ya mara kwa mara kati ya wavuvi na watu wa uhifadhi.

Juhudi za kunusuru ziwa

Katika kulinusuru ziwa hili, yako baadhi ya mambo yanafanyika ili kulihifadhi, kulilinda lakini pia kulizuia matumizi yasizidi uwezo.

Benson Mwaise, Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge (Burunge WMA) amesema ukame unaotokea mara kwa mara husababishwa na mabadiliko ya tabianchi na unaweza kuzuilika kupitia utunzaji wa mazingira kwa ajili ya bioanuai za viumbe vyote.

Mwaise aliwaambia hivyo waandishi wa habari wanaoshiriki mafunzo maalum ya uhifadhi ya Bionuwai yaliyofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani(USAID), waliotembelea ushoroba wa Kwakuchinja.

Anasema kuwa katika kulinda ziwa kuna mipaka ambayo wameweka linaloruhusiwa kuvua samaki lakini pia lipo eneo ambalo wamezuia kuvua ili samaki wanapopungua wabaki kwa ajili ya kuzaliana.

“Ukame ukizidi maji hubakia katika eneo dogo lililoko hifadhini na samaki nao hupungua hivyo tunalazimika kulifunga ziwa kwa muda wa miezi minne hadi sita kutoa nafasi wachache waliobakia kuzaliana kuendeleza kizazi ili kunusuru shughuli za uvuvi ziwani maji yatakapojaa,” anasema Mwaise.

Wataalam watahadharisha matumizi ya kemikali 

Matumizi ya mbolea za viwandani na viutatilifu kwenye kilimo siyo hatari kwa samaki pekee bali wanyama wote wanaozunguka hifadhi.

Mtaalamu wa Ikolojia nchini, Yustina Kiwango, aliyewahi kukaimu nafasi ya Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara amesema kuwa maji ya ziwa hilo lenye magadi na wingi wa madini ya Fosforas huzimwa pia na kemikali hizo.

 “Kuna ambao hawafi lakini wanakuwa dhaifu na wengine wanaathirika mfumo wa umeng’enyaji chakula na kukosa madini aina ya kalsiam na fosforas na kusababisha kutaga mayai yenye maganda dhaifu ambayo hayatotoleki vifaranga vya flamingo hivyo kizazi hakiendelei,” amesema Yustina na kuongeza;

“Hapa ndio mfumo mzima wa Ikolojia inapoharibika kwa kuathirika kwa wanyama wengine ambao wanategemea ndege hao wazaliane kwa kitoweo.”

Yustina wananchi wasilime eneo la ziwa ili kupunguza hatari ya kuathiri bioanuai zilizopo katika eneo hilo.

Kwa yale maeneo yanayozunguka ziwa, amesema wafanye kilimo rafiki ikiwemo  kutumia mbegu za asili, mbolea vunde, au samadi za wanyama na pia kutumia dawa za asili kama utupa, muarobaini na pilipili kwa ajili ya kuulia wadudu waharibifu.

 Makala hii ni sehemu ya mafunzo ya uandishi wa habari za bioanuai yaliyofadhiliwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) chini ya mradi wa Tuhifadhi Maliasili. 

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari