Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Binadamu wanavyotishia Mapito ya Wanyamapori katika eneo la Kwakuchinja, Manyara

Miaka 34 iliyopita wakati Saimoni  Silas anahamia katika Kijiji cha Mwada kilichopo wilayani Babati, alikuwa na mke na watoto wawili pekee.

Nyumba moja iliwatosha kulala lakini sasa ana watoto tisa na eneo hilo bila kuongeza makazi lisingetosha tena kuishi na familia yake. 

“Mimi nilihamia hapa mwaka 1989 nikiwa na mke na watoto wawili wa kiume ambapo nyumba moja pekee iliyokuwa na vitanda viwili ilinitosha kabisa,” anasema.

Kipindi hicho Babati ilikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Arusha, hivi sasa ni moja ya wilaya za Mkoa wa Manyara baada ya kugawanywa mwaka 2003.

Kwa sasa eneo analoishi Silas lina nyumba sita. Tayari yeye ana watoto tisa kati yao wa kiume ni sita, na wa kike watatu.

Saimon Silas ambaye sasa ana miaka 62 anasema kuwa kutokana na kuongezeka kwa familia yake nyumba za makazi alizojenga ndani ya  ushoroba wa Kwakuchinja wilayani Babati mkoani Manyara zimeongezeka hadi kufikia sita.

“Kwa sasa kuna nyumba sita hapa yenye watu 20 huku watatu wakiwa nje kimasomo,” anasema na kuongeza…

“Watoto wangu wakubwa watatu wa kiume kila mmoja amejenga nyumba na anaishi na familia yake akiwemo mkubwa anayeitwa Elisha (36) ana mke mmoja na watoto wanne anaefuata ni Raymond (34) mwenye mke mmoja na watoto watatu, huku Ernest aliyezaliwa hapa hapa mwaka 1992 tayari naye ana mke na mtoto mmoja.”

Kisa cha Silas ni moja ya masimulizi ya maelfu ya wakazi wa vijiji 10 vilivyoko ndani ya kata tatu, ndani ya hifadhi ya ushoroba wa kwakuchinja ambao unazidi kulemewa na ongezeko la makazi na kusababisha uhalisi wake kupotea.

Ushoroba huo ulioko katikati ya hifadhi za Tarangire na Manyara uhalisia ni njia au mapito ya Wanyamapori tangu enzi na enzi.

Wanyamapori katika eneo la vilima vitatu huku makazi ya watu yakionekana kwa mbali nyuma (Picha na Berry Mollel)

Hata hivyo, kutokana na ongezeko la watu na makazi, eneo hilo limeendelezwa kwa kilimo na ufugaji pamoja na uwekezaji wa miundombinu mbalimbali ya biashara hali inayoiweka hifadhi hiyo hatarini kutoweka.

Makazi ilivyoutafuna ushoroba wa Kwakuchinja

Meneja wa Taasisi ya Chem chem Martin Mung’ong’o iliyoko ndani ya hifadhi ya ushoroba wa Kwakuchinja iliyojikita katika utoaji wa elimu ya uhifadhi wa wanyama pori aliwaambia waaandishi wa habari kuwa shughuli hizo zimeathiri kwa kiasi kikubwa ushoroba huo. 

“Njia hiyo ni asili ya wanyamapori ambayo kwa sasa ina ukubwa wa Kilomita za Mraba 283 pekee, miaka ya nyuma ulikuwa na ukubwa wa zaidi ya kilometa 600 za Mraba  zilizokuwa zimeainishwa miaka ya 80,” Mung’ong’o aliwaambia waandishi wa habari.

Waandishi hao ni wale wanaoshiriki mafunzo maalum ya uhifadhi ya Bionuwai yanayoendeshwa na kampuni ya habari na Teknolojia ya Nukta Afrika  kwa ufadhili wa shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), waliotembelea ushoroba wa Kwakuchinja.

 Alisema kipindi hicho, Kwakuchinja zaidi ya kuunganisha Tarangire na Manyara, ushoroba huo pia ulijumuisha baadhi ya nyanda za Serengeti na Ngorongoro.

 “Ushoroba wa Kwakuchinja enzi hizo ulianzia eneo la Makuyuni, wilayani Monduli Mkoani Arusha hadi mbele zaidi ya sehemu iitwayo Mbuyu wa Mjerumani, wilayani Babati, katika mkoa wa Manyara” anasema na kuongeza…

“Kwa sasa zaidi ya kilomita za mraba 317 zimemegwa na makazi ambao katika kujiendeleza wamefanya uwekezaji wa aina mbali mbali ikiwemo kilimo, ufugaji na majengo ya biashara” anasema Mung’ong’o.

Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022 kutoka tovuti ya ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Kata za Mwada, Nkaiti na Magara vilivyopo ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja zilikuwa na jumla ya wakazi 49,946.

Jitihada za Kuyanusuru mapito ya Kwakuchinja

Kutokana na kuwa katika hatari ya kutoweka, wadau mbali mbali wamejitokeza kutaka kujaribu kuinusuru ushoroba huo ambapo kwa sasa umehifadhiwa kupitia juhudi za utunzaji wa mazingira unaotekelezwa na Jumuiya za hifadhi za kijamii za Burunge na Randileni, pamoja na shamba la Manyara.

Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge inaundwa na vijiji 10 katika kata za Mwada, Magara na Nkaiti ambavyo baadhi vina hati za kimila.

Katibu wa Jumuiya ya Burunge, Benson Mwaise anasema vijiji vinashirikiana kuhifadhi eneo la mapito ya Wanyama.

“Pia wanavijiji wananufaika kwa sababu wameweza kuingia katika mikataba na makampuni kadhaa yanayoendesha shughuli za utalii wa picha na hoteli katika hifadhi ya Burunge,” alifafanua Mwaise.

Kutokana na mapato ya shughuli za kitalii, Burunge inaweza kugharamia shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na uoto wa asili katika eneo la mapito ya Wanyama ndani ya uwanda wa Tarangire-Manyara.

Jamii na Uhifadhi Shirikishi

Pamoja na kupata fedha kutokana na utalii, Burunge pia inatekeleza miradi yake kwa ufadhili wa USAID kupitia mradi wake wa ‘Tuhifadhi Maliasili’. Baadhi ya mapato wanayopata kutokana na shughuli za kitalii na uwekezaji kutoka katika eneo hilo huviwezesha vijiji wanachama wa hifadhi kujipatia kipato, ambapo kila kijiji hupewa zaidi Milioni 100 kila mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

“Kwa minajili hiyo, wananchi hupata mwamko wa kushiriki katika masuala ya uhifadhi pamoja na vita dhidi ya ujangili badala ya kuuharibu,” alisema Mwaise

 Vile vile wanawake wa maeneo ya Hifadhi ya jamii ya Randilen sasa wanaweza kutengeneza bidhaa za mapambo kwa ajili ya kuwauzia watalii wa kigeni kupitia taasisi ya ‘Asilia Giving,’ kwa kushirikiana na Utafiti wa Simba Tarangire pia kupitia ufadhili wa USAID Tuhifadhi Maliasili.

Zakaria Israel, ambaye ni afisa mradi wa Shirika la Asilia Giving anasema wanawake wa maeneo hayo wamenufaika vilivyo na mradi huo na wengi wameweza kuwasomesha watoto na hata kujenga makazi.

 “Katika kutunza uhifadhi, ilibidi tuwalete wanawake pamoja katika kuwatafutia kingine cha kufanya kuingiza kipato tofauti na kukata miti na kuchoma mkaa na tunashukuru Mungu wameelewa sasa ni watunzaji wazuri wa mazingira”alisema Zakaria

Wataalam wanasemaje?

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tafiti katika taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania, Dk Julius Keyyu, Kwakuchinja ni moja ya shoroba 41 ambazo ziko hatarini kutoweka nchini.

Dk Keyyu anasema kuwa hadi mwaka 2022, Tanzania ilikuwa imeziorodhesha jumla ya shoroba 61, katika maeneo mbalimbali nchini

“Lakini, kati ya shoroba zote 61, Tanzania ni mbili tu ndizo zimesajiliwa rasmi,” alisema mtaalamu huyo wa Utafiti na kubainisha kuwa Kwakuchinja pia sio moja ya shoroba zilizosajiliwa rasmi.

Dokta Keyyu anasema kuwa moja ya hizo Shoroba mbili zilizosajiliwa na kuorodheshwa katika Gazeti la Serikali ni ile ya Kitendeni, inayounganisha Pori la Longido na uwanda mpana wa West Kilimanjaro, magharibi mwa mlima mrefu zaidi barani Afrika.

Ushoroba mwingine uliosajiliwa rasmi ni ule wa Igando-Igawa unaoziunganisha hifadhi za Ruaha na Pori la akiba la Mpanga-Kipengere, kusini mwa Tanzania.

“Lakini pamoja na kusajiliwa, ushoroba wa Igando-Igawa uko katika hali mbaya sana na ukihitaji kunusuriwa,” alisema mtafiti huyo wa TAWIRI.

 Alisema kuwa kuanzia sasa shoroba zote nchini ikiwemo ya Kwakuchinja zinahitaji juhudi za makusudi serikali kuokoa katika hatari ya kutoweka ili kupunguza migongano ya wanyama pori na binadamu lakini pia kuendeleza uhifadhi wa bionuwai za wanyama na kuwanusuru katika hatari ya kutoweka nchini.

Pale Serikali inapojikita kuzinusuru shoroba nchini

Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii imeliona hatari ya kutoweka kwa shoroba hizo ikiwemo kwakuchinja ambapo hivi karibuni Waziri mwenye dhamana Angela Kairuki akizungumza jijii Arusha kwenye mkutano wa wataalamu wa wanyama pori na mali asili kutoka nchi za Afrika alisema kuwa serikali imetenga bajeti ya kuandaa mpango wa kunusuru hilo.

Alisema serikali sasa imeona umuhimu wa kutunza mapito ya wanyama na iko katika hatua za kuzinusuru shoroba zote zilizoko hatarini kutoweka.

Alisema wizara yake kwa kushirikiana na wizara ya ardhi itaanda mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya shoroba kwa kuzingatia matokeo ya tafiti zilizofanywa na wataalamu wa wanyamapori.

“Tayari tumetenga fungu maalum kwa ajili ya mradi huo na utekelezaji wake, ikiwemo kuainisha na kuchora mipaka ya shoroba na unaanza wakati wowote kuanzia Januari 2024,” alifafanua Waziri Kairuki katika kikao hicho.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari