Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Moto Kilimanjaro: Vikosi vya Jeshi la Wananchi vyaingia Kazini Moshi

Moto umekuwa ni gumzo katika mlima mrefu barani afrika

Vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania vimetua mjini Moshi tayari kujumuika kwenye shughuli nzito ya kuzima mioto iliyolipuka katika maeneo ya Mlima Mrefu kuliko yote Barani Afrika.

Moto uliolipuka takriban wiki mbili zilizopita unaendelea kuteketeza maeneo muhimu ya Kilimanjaro na sasa imebidi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lijitose kwenye operesheni ya kuuzima.

Taarifa kutoka kitengo cha mawasiliano cha JWTZ inasema kuwa hii ni katika kutekeleza amri ya Mkuu wa majeshi ya Ulinzi Nchini, Jenerali Jacob John Mkunda.

“Jeshi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa kufuatia janga la moto unaoendelea kuwaka ndani ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda ameamuru JWTZ kushiriki operesheni ya kuzima moto huo unaoendelea kusambaa.”

Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda – Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tayari Maafisa na Askari wa JWTZ wamewasili maeneo ya Siha na Mwika Mkoani Kilimanjaro ili kuanza rasmi Operesheni ya uzimaji wa moto katika mlima Kilimanjaro.

Luteni Kanali Ilonda anabainisha kuwa Jeshi la Wananchi litashirikiana kikamilifu na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, Wadau mbalimbali na Wananchi katika kazi hiyo.

“Hii ni ili kuhakikisha moto huo unadhibitiwa mapema kabla ya kuleta madhara makubwa katika Hifadhi hiyo. Aidha, JWTZ litaendelea kusaidia Mamlaka za kiraia pale litakapohitajika kufanya hivyo.”

Moto ulianza kueteketeza maeneo ya mlima kilimanjaro usiku wa kuamkia Jumamosi ya Tarehe 22 Oktoba 2022.

Taifa Tanzania iliripoti sakata hilo.

Tangu wakati huo tatizo hilo limekuwa likiendelea mlimani na inadaiwa kuwa upepo mkali unachangia kuchochea na kusambaza miale ya moto kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Maelfu ya watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani hupanda mlima Kilimanjaro kila mwaka.