Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Tanga, Arusha, Kilimanjaro kuwa gizani zaidi

Mikoa mitatu ya Kanda ya Kaskazini, yaani Tanga, Arusha na Kilimanjaro itaathirika zaidi na mgawo wa umeme unaoikabili nchi nzima kwa sasa.

Taarifa kutoka shirika la umeme inadai kuwa hii yote ni kutokana na ukame mkubwa unaoikumba Tanzania.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mabwawa ya kuzalisha umeme ya Hale, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Pangani yenye uwezo wa kuzalisha megawati 266 za umeme yamepungua uwezo wake kwa kiasi kikubwa.

Shirika la umeme, yaani Tanesco, linasema kuwa mabwawa hayo kwa sasa yanazalisha megawati 34 za umeme tu.

Kutokana na hali hiyo, kuna upungufu mkubwa wa nishati ya umeme.

Upungufu huo ndio unadaiwa kuathiri upatikanaji wa umeme wa kutosha katika sehemu mbalimbali za nchi.

Lakini mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga ndio itaathirika zaidi.

“Kutokana na ukame huu mkubwa, mikoa hii inalazimika kupata umeme wake kutoka katika vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia vilivyopo Dar Es Salaam,” Tanesco inadai.

Aidha kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa shughuli za uchumi na viwanda katika mikoa hiyo, njia za kusafirishia umeme kutoka Dar Es Salaam kwenda kwenye mikoa hiyo zimezidiwa na hivyo kusababisha umeme unaopatikana katika mikoa hiyo kutokidhi mahitaji.

Shirika la Umeme

Sasa tunafanyaje?

lli kutatua kadhia hii, Shirika la umeme nchini linasema kuwa linachukua hatua zifuatazo;

Kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Luguruni ili kuhudumia maeneo yote kati ya Luguruni mpaka Chalinze na hivyo kutoa nafasi ya umeme mwingi zaidi kufika katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Hii itasaidia kupunguza mzigo wa umeme katika njia ya sasa inayotoka Ubungo hadi Chalinze na hivyo kuruhusu umeme mwingi kwenda katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Kujenga njia mpya kutoka kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Lemugrul kilichopo Kisongo jijini Arusha.

Hatua hil itapunguza mzigo wa umeme unaopitia kwenye kituo cha Njiro hivyo kuongeza kiasi kingine cha umeme kufika katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kupitia Arusha.

Hii ni kutatua tatizo la sasa la Arusha ambapo kituo cha Njiro kinapitisha umeme wa Kilimanjaro na Tanga na hivyo kuzidiwa na kusababisha umeme kutokidhi mahitaji katika mkoa wa Arusha.

Hali ya ukame mkubwa ilitabiriwa kutokea mwaka huu na Shirika limechukua hatua za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vituo vyake vya gesi, kazi katika upanuzi wa kituo cha Kinyerezi 1 imefikia ukingoni na inategemewa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu ili kuingiza megawati nyingine 185 katika Gridi ya Taifa.

Megawati 90 kati ya hizo zipo kwenye majaribio hivi sasa. Hatua hii itaimarisha uwezo wa kukabiliana na upungufu wa maji ambao unategemewa kuendelea.

Pamoja na kazi zote hizi kuendelea kufanyika…..

Ofisi za Tanesco mikoani zimeagizwa kutoa ratiba ya upungufu wa umeme kwenye maeneo yote yanayoathirika na wakazi kupewa taarifa kwa njia mbalimbali pamoja na ujumbe mfupi wa maneno kwenda kwa mhusika wa eneo hilo litakaloathirika.