Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Param Kilimanjaro, Kompyuta Kubwa zaidi nchini Tanzania yaongezewa nguvu ya jua kutoka India

India, kupitia Ubalozi wake jijini Dar-es-salaam imeikabidhi Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia (NM-AIST) jumla ya betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane.

 Berti hizo zimetolewa mahsusi kwa ajili ya kuiwezesha kompyuta kubwa zaidi Afrika Mashariki ambayo sasa itakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa zaidi ya saa 24 hata pale ambapo kutatokea hitilafu ta umeme.

Kompyuta hiyo kubwa zaidi nchini ijulikanayo kama ‘Param Kilimanjaro,’ ina uwezo mkubwa wa kuchakata data kwa kasi na ufanisi mkubwa na ilifungwa katika chuo kikuu cha Nelson Mandela mwaka 2016.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Profesa Anthony Mshandete, alisema kompyuta hiyo inauwezo wa kuchakata data kwa kasi ya hali ya juu na tangu ilipozinduliwa miaka sita iliyopita ilikumbana na changamoto ya nishati pale umeme unapokatika.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ubunifu Profesa Anthony Mshandete (katika) pamoja na Balozi wa India Nchini Tanzania Binnaya Srikanta Pradhan (Kulia) wakikata utepe kuashiria mapokezi rasmi ya Betri 64 zenye uwezo wa kuhifadhi nishati jua kwa saa nane kutoka Serikali ya India.

Alisema upatikanaji wa Betri hizo utawezesha kompyuta hiyo kufanya kazi kwa ufanisi kwa manufaa ya taasisi ambapo hutumika kwa ajili ya kufundisha shahada ya pili ya (Master’s Degree) , kuchakata data za Kibailojia pia itatumika kuchakata data kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na itasaidia katika kuhifadhi data nyeti za serikali.

“Kompyuta hii itasidia kuhifadhi data ndani na nje ya Tanzania kwani inauwezo mkubwa katika ufanisi wenye tija katika masuala ya Tehama, na tunashukuru kwa betri hizi ambazo zitawezesha upatikanaji wa uhakika wa umeme katika kufundishia masomo mbalimbali chuoni hapa “Anasema Profesa Mshandete.

Kwa upande wake Balozi wa India nchini Tanzania, Binnaya Srikanta Pradhan alikipongeza kituo cha Umahiri cha Teknolojia Afrika Mashariki, katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kutoa elimu zaidi katika masuala ya TEHAMA (ICT).

Alisema India inatambua mchango mkubwa wa masuala ya teknolojia na kuipongeza taasisi hiyo kwa kutoa elimu katika masuala ya kompyuta.

“India itaendelea kuhakikisha masuala ya Tehama yanakua zaidi na chuo hiki ni sehemu ya kutoa elimu ya Tehama kwani Dunia hii ina mabadiliko mengi katika masuala ya TEHAMA, nawapongeza kwa kuimarisha masuala ya teknolojia ” Alisema Balozi Pradhan.

Awali India ilitoa kompyuta nyingine kubwa kwa ajili ya Taasisi ya Teknolojia jijini Dar-Es-salaam (DIT), ingawa hiyo iitwayo Param Serengeti haifikii uwezo wa Param Kilimanjaro iliyopo NM-AIST Arusha.

Naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Masuala ya Tehama, Hesabati na Mawasiliano Dk, Judith Leo aliishukuru Serikali ya India kwa kuendeleza Ushirikiano na Kituo hicho na kwa kuwezesha upatikanaji betri utakaosaidia Kompyuta hiyo kubwa (Super Computer).

Kompyuta hiyo inaweza kufanya kazi za tafiti kufanya kazi kwa bidii kwani awali walikuwa na changamoto ya umeme pale wanapotaka kufanya kazi zao, lakini sasa uwepo wa betri hizo utawezesha ufanisi zaidi katika utoaji wa mafunzo kwakutumia kompyuta hiyo.