Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

‘Sisi ndio tulitoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro!’

Wakazi wapatao 2000 kutoka vijiji saba vinavyouzunguka uwanja wa ndege wa kimataifa wa kilimanjaro, wanadai kuwa baba na babu zao ndio hasa waliowezesha uwepo wa eneo hilo la kutua ndege.

“Waanzilishi wa vijiji vyetu ndio walitoa eneo kwa serikali ili uwanja wa ndege wa KIA uweze kujengwa mwaka 1971,” walibainisha wanavijiji hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika moja ya vijiji hivyo.

Mkutano huo ulilenga kujadili mgogoro uliodumu kwa muda mrefu, baina ya wakazi wa maeneo yanaouzunguka uwanja wa ndege Kilimanjaro na Shirika la Umma lenye mjukumu ya kuendesha uwanja huo, yaani KADCO.

“Sisi ndio tulitoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege!”

Hii ni kufuatia ziara ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliyoifanya hivi karibuni ambapo alitamka kuwa serikali ya mkoa inafanya utaratibu wa kupima upya maeneo yanayozunguka uwanja.

Babu aliongeza kuwa zoezi hilo linalenga kutambua maeneo halisi yanayomilikiwa na wananchi na eneo ambalo linapaswa kuwa chini ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Tarehe 11 Novemba 2022 ndio siku iliyopangwa kuwekwa mawe ya kuainisha mipaka ya uwanja.

Hata hivyo wanavijiji wanahisi kuwa kuna njama za kuwaondoa katika maeneo yao halali kwa madai ya kuvamia uwanja wa ndege.

“Sisi huu uwanja umetukuta, Unajengwa tunauona. Na sio hivyo tu, ardhi ambayo imetumika kuwekeza uwanja tulitoa sisi ili uweze kujengwa,” anasema mmoja wa wanavijiji, Jacob Pallangyo.

Vijiji saba vinavyouzunguka uwanja huo ni pamoja na Sanya station, Mtakuja, Tindigani, Chemka, Majengo, Malula na Samaria.

Maeneo hayo yana wakazi zaidi ya 20000 ambao wanamiliki mifugo zaidi ya Laki Moja.

Pia kuna Shule 18 za Msingi na Sekondari, Zahanati, Makanisa kadhaa na Misikiti, pamoja na majengo ya biashara na nyumba za wanavijiji.

Mkazi mwingine, Elia Mollel anabainisha kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro hakusikiliza hoja za wananchi walizoziwakilisha kupitia risala waliyosoma mbele yake.

“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hili,” walisema wanavijiji.

Wakazi hao wa eneo la KIA wamemuomba rais kusitisha zoezi la uwekaji mawe ya mipaka hadi pale kamati maalum inayoshughulikia mgogoro huo itakapokuja kuzungumza na wananchi.

Kamati hiyo inaongozwa na Mwenyekiti wake, Angelina Mabula, ambaye ni waziri wa ardhi. 

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro, ambao ni wa pili kwa ukubwa baada ya ule wa Dar-es-salaam, ulifunguliwa rasmi Desemba 1971 na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere.