Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Vijana 150,000 hujiunga na vyuo vya Ufundi Stadi Kila Mwaka nchini Tanzania

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), limefungua rasmi dirisha la udahili wa wanafunzi wapya kwa mwaka 2023 nchini, huku idadi ya vijana katika vyuo hivyo ikielezewa kuongezeka.

Wakati huo huo vyuo vya ufundi nchini vimepewa angalizo dhidi ya vitendo vya kuingilia mchakato wa udahili wa wanafunzi.

Vyuo hivyo vimeonywa kuwa jaribio lolote la kujaribu kuharibu taratibu zilizowekwa litavigharimu vyuo hivyo.

Mkurugenzi Uthibiti, Ufuatiliaji na Tathmini wa NACTVET, Dk Jofrey Oleke, akitangaza kuanza kwa udahili  kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada, katika kozi zinazotolewa na vyuo mbalimbali nchini kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Dk Oleke amesema endapo kuna chuo kitakiuka masharti ya udajili hawatasita kukichukulia hatua kali kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

“Kabla ya ufunguzi wa udahili,tulikaa na vyuo vyote ambavyo vinahusika na udahili wa wanafunzi katika kada hii ya kati na tukakubaliana na yeyote atakayehusika kuharibu mchakato wa udahili atasitishiwa udahili wa mwaka huu kwa hiyo vyuo vinatahadharishwa kuhakikisha vinazingatia taratibu za udahili kama ilivyoelekezwa,” amesema

“Baraza linawashauri waombaji,wazazi na walezi kuhakikisha wanaoomba vyuo ambavyo vimeorodheshwa kwenye kitabu cha mwongozo wa udahili mwaka wa masomo 2023/2024, mwongozo unaopatikana kwenye tovuti ya baraza.”

Wastani wa vijana 150,000 hujiunga na vyuo vyaufundi stadi kila mwaka nchini Tanzania.

Kuhusu kuanza kwa udahili, Dk Oleke amewataka wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga na kozi ngazi za Astashahada na Stashahada, kufanya maombi yao kwa umakini ili kapata nafasi ya kujiunga na programu ambazo watatimiza vigezo vyake.

“Udahili huo unaanza Mei 21, 2023 hadi Juni  30, 2023 katika awamu ya kwanza.” Alisema.

Hata hivyo wanafunzi wanaotaka kujiunga na programu za afya na sayansi shirikishi, upande wa Tanzania Bara wao wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia udahili wa pamoja (Central Admission System-CAS) katika tovuti ya baraza.

“Tunawatahadharisha waombaji wa nafasi mbalimbali katika vyuo vya elimu ya ufundi wahakikishe wanafahamu vyuo vilivyosajiliwa na baraza na programu ambazo zeye ithibati na kuandika taarifa zao sahihi,” alisema.

Wanafunzi au wazazi wameombwa pia kutunza taarifa watakazopatiwa na Baraza bila kumpatia mtu yoyote ili kuepusha usumbufu katika zoezi zima la maombi ya kujiunga na vyuo au programu mbalimbali,”

Akingumzia Hilo, mmoja wa wazazi Onesmo Laizer alisema kuwa wamefurahia kupata maelezo ya udahili kutoka kwa wahusika wenyewe kwani wamekuwa wakipitia utapeli wa Mara kwa mara kwa madalali ambao huishia kuwalia hela zao kupata nafasi.

“Utapeli wa udahili umekuwa mwingi tunaomba NACTVET wajaribu kudhibiti utapeli huu kwani umekuwa ukiwagharimu wazazi wengi kwa madai wanakusaidia kumdahili mwanafunzi wako na mwisho baadae mtoto anakosa nafasi na ameshakula hela mwisho Hana la kukusaidia” alisema