Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Wafugaji Waomba Kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan

Wafugaji Asili, Warina asali na wananchi wengine kutoka jamii za pembezoni wanaomba kukutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ili nao wapate fursa ya kuwakilisha masuala yanayowahusu yakiwemo malalamiko kwa kiongozi wa nchi.

Wakizungumza mkoani Arusha, katika mkutano maalum, wananchi hao kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaelezea wasiwasi wao kwamba huenda kiongozi wa nchi hapewi taarifa sahihi kuhusu maisha yao na shughuli wanazofanya ili kuishi.

Katika mkutano wao wa pamoja ambao ulihusisha pia Asasi za kiraia na zile zinazotetea haki za binanadamu na utawala bora, wananchi hao waliomba kupewa fursa ya kukutana na kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan ile aweze kusikia moja kwa moja kutoka kwao.

Moja ya malengo ya wananchi hao kutaka kukutana rasmi na Rais Samia ni kumpa taarifa kamili na hali halisi juu ya migogoro ya ardhi inayoendelea katika maeneo mengi nchini.

“Hivi sasa kuna watu wanaotoa taarifa nyingi zisizo sahihi zinazopotosha kuhusu jamii za kifugaji na masuala ya uhifadhi nchini. Na hii ndio husababisha migogoro mingi isiyo ya lazima katika maeneo ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Nyanda za Juu Kusini,” walifafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika linalojihusisha na maendeleo ya jamii za wafugaji (PALISEP), Robert Kamakia anabainisha kuwa kuna tafsiri nyingi potofu, pamoja na taarifa lukuki za uongo kutoka kwa viongozi kuhusu wafugaji na jamii nyingine za pembezoni.

“Migogoro mingi hutengenezwa makusudi kuwachonganisha baadhi ya watanzania na serikali ili wanufaike kupitia matatizo au hali ya sintofahamu inayojitokeza,” alifafanua Kamakia.

Yeye anaamini kuwa iwapo wananchi husika pamoja na asasi za kijamii zitakutana na Rais Samia basi asilimia kubwa ya matatizo yanayoikabili sekta za ufugaji, uhifadhi na maliasili yatatatuliwa moja kwa moja.

Naye Loserian Maoi, ambaye ni mkurugenzi wa shirika la INDIGO (Integrated Development Initiative in Ngorongoro) alisema haiwezekani kuwa kila vurugu kuhusiana na ardhi zinapotokea basi lazima jamii za kifugaji ziwe ndio wahanga.

“Na ikumbukwe kuwa sekta ya ufugaji pia ina mchango mkubwa sana katika maendeleo na uchumi wa taifa, hivyo ni muhimu wafugaji wakaheshimiwa na shughuli zao kupewa kipaumbele kama vile ambavyo sekta za uhifadhi na viwanda zinavyothaminiwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Maoi haiwezekani kwamba maeneo yote ya wafugaji nchini yageuzwe kuwa hifadhi wakati sekta ya mifugo inatoa mchango mkubwa wa kiuchumi kwa taifa na halitengenezewi mazingira mazuri ya ufugaji wao.

Mtaalamu wa sheria, wakili Alais Melau alisema wanamfano hai wa jinsi serikali haiheshimu mihimili mingine akitolea mfano kijiji cha Mobegere kilichopo Morogoro ambapo mahakama ilitoa hukumu na ikawapa hati wafugaji ya kuishi eneo hilo lakini serikali ilichokifanya ni kufuta kijiji hicho.

Sambamba na hayo, Mary Mushi kutoka shirika la kuhudumia akina mama na watoto, yaani Women and Children Welfare Support, anasema pamekuwa na matukio ya kupigwa mnada na uuzwaji wa mifugo ya watu masikini bila huruma.

Mifugo hiyo, kwa mujibu wa Mary Mushi hukamatwa pale inapopita ndani au hata karibu ya maeneo ambayo awali yalikuwa ni kwa ajili ya mifugo lakini kukawa na mabadiliko ya matumizi ya ardhi.

Mara nyingi wanyama hao huwa wamezoea kwenda sehemeu hizo na wao hawajui kuwa maeneo hayo yamebadilishiwa matumizi hivyo kukamatwa na kuuzwa.

“Mifugo hiyo wakati mwingine huelekea maeneo hayo ikiwa peke yake na inapoonekana basi hudaiwa kuwa haina mwenyewe. Ikumbukwe kuwa hayo huwa ni maeneo yaliyobadilishwa matumizi ambayo awali yalikuwa yakitumiwa na wafugaji.”

Hali hii mara nyingi ni jambo linaloongeza umaskini na kuhatarisha ustawi wa wanawake na watoto.

Mary aliongeza kuwa mnamo tarehe 28 Mei 2018 bunge lilipitisha kuwa serikali isiweke vigingi kwenye maeneo yote yenye migogoro ya ardhi badala yake itumie taratibu za kisheria lakini agizo hilo limepuuzwa na vigingi viliendelea kuwekwa maeneo mbalimbali.

Aliongeza kuwa moja ya upuuzwaji wa agizo hilo ni uwekaji wa vigingi kwenye eneo linalopakana na uwanja wa ndege wa Kilimanjaro KIA licha ya wananchi hao kuwa na hati ya umiliki ardhi ambayo ilipatikana kabla ya uwepo wa uwanja huo.

Unaweza pia kusoma habari hii katika lugha ya Kiingereza Hapa

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari