Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Vitambulisho vya Taifa Sasa kuombwa Mtandaoni

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanzisha Mfumo wa Usajili wa Watu kwa njia ya Mtandao (Online Registration).

Mamlaka inadai kuwa huu ni mfumo utakaowezesha wananchi wenye sifa za kuomba Vitambulisho vya Taifa kujaza fomu mtandaoni popote walipo. Lakini Watanzania wengi hawaoni nafuu yeyote.

Kwa mujibu wa NIDA watu wataomba vitambulisho popote walipo bila kulazimika kwenda Ofisi za Usajili za Wilaya au vituo vya Usajili vya NIDA.

Ili kujisajili mwombaji ataandika eonline.nida.go.tz katika mtandao wa internet na kufuata maelekezo.

Mamlaka inadai kuwa mfumo huu unalenga kupunguza usumbufu kwa waombaji wa Vitambulisho vya Taifa ambao kwa sasa wanalazimika kufika ofisi za NIDA kuchukua fomu za maombi ya Vitambulisho vya Taifa.

NIDA wanadai kuwa kupitia mfumo huu ujazaji wa fomu na kuweka viambatisho utafanyika mahali popote kwa kutumia kifaa chenye uwezo wa kupokea mtandao wa mawasiliano (intaneti).

Lakini baadhi ya watu waliohojiwa wanasema usumbufu bado uko palepale kama haujaongezeka.

Hii ni kwa sababu baada ya kujaza fomu, mwombaji atatakiwa tena kuchapisha hiyo fomu (print) na kuipeleka Serikali ya Mtaa anapoishi kwa ajill ya kuthibitisha ukaazi wake.

Isitoshe, mtu atalazimika tena kusafiri hadi zilipo ofisi za NIDA kwa ajili ya kuwasilisha makaratasi hayo.

Pia muombaji analazimika kupeba nakala lukuki za viambatanisho kwenye Ofisi ya NIDA iliyoko katika wilaya anayoishi ingawa tayari nakala za uthibitisho wake alikwisha kuzipakia mtandaoni.

Mwombaji pia atalazimika kuhojiwa na Uhamiaji, kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole.

“Mfumo huu utapunguza muda unaotumika katika kusajili taarifa za mwombaji kwa kuwa usajili wa taarifa za mwombaji utakuwa umefanywa na mwombaji mwenyewe,” wanadai NIDA.

Pamoja na kurahisisha huduma ya usajili kwa raia na wageni wakaazi, utapunguza pia gharama zinazotumika katika kuchapisha fomu za usajili na gharama za uchakataji wa taarifa.

Aidha, usajili kwa njia ya Mtandao utaongeza idadi ya Watu wanaojisajili kwa kuwa huduma hiyo itapatikana mahali popote badala ya kufika katika Ofisi ya NIDA kufuata huduma hiyo.

Unaweza pia kusoma habari hii katika lugha ya KIINGEREZA