Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Zaidi ya wanafunzi 50 Ngorongoro wawezeshwa kujiunga sekondari kwa michango ya wananchi

Ngorongoro

Wanafunzi Hamsini na Moja (51) ambao wanatoka kwenye familia zisizojiweza kiuchumi lakini wamefaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari, wamewezeshwa kwenda shule kupitia michango ya wananchi.

Watoto hao watakaojiunga na elimu ya sekondari mwaka huu, kwa kidato cha kwanza, baada ya kuhitimu elimu ya msingi, ni kutoka katika kata tatu za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, mkoani Arusha.

Wanafunzi hao wamepewa misaada ya vifaa na mahitaji mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 12 ili kuwawezesha kuhudhuria masomo katika shule za sekondari.

Vifaa walivyokabidhiwa wanafunzi hao ni pamoja na magodoro, masanduku ya kubebea nguo mahitaji na vifaa vya shule, mavazi ya shule, viatu, mikebe (Geometry Sets) mashuka, vitabu na madaftari.

Pamoja na hayo wamepewa vifaa vingine pia kama kalamu, ndoo, karatasi nyeupe za kuchapishia (white paper rims), vifaa vya afya na usafi zikiwemo sabuni, taulo za kike, na mahitaji mengine muhimu.

Bidhaa zote hizo vimetokana na michango mbalimbali ya wananchi na wadau wengine wa maendeleo wilayani Ngorongoro na maeneo ya jirani.

Lengo ni kuwasaidia wanafunzi hao waweze kuendelea na masomo ya sekondari.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Ngorongoro, Mohamed Bayo almaarufu Marekani alisema wanafunzi waliopata msaada huo wanatoka katika familia duni kutoka kata za Orgosorock, Enguserosambu na Oloirien.

Wanafunzi wakiwa tayari kwenda shule

Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Bayo aliwataka wanafunzi  hao wa kike wasiende kurubuniwa kwa mapenzi hali itakayowafanya washindwe kuendelea na masomo.

“Nyie mnatoka katika familia ambazo zina changamoto hivyo mnatakiwa mkasome kwa bidii ili baadaye mje msaidie wazazi wenu,” alisema.

Alisema utaratibu wa kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia duni umeanza tangu 2021 baada ya kuanzishwa kwa mfuko maalum wa diwani wa kata ya Orgosorock.

Bayo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Orgosorok alisema mfuko huo tangu umeanzishwa umesaidia jumla ya wanafunzi 104 waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari za serikali na kiasi cha zaidi ya Shilingi Milioni 24 zimekwisha kutumika.

Aliongeza kuwa mfuko huo ambao pia unaundwa kwa kushirikisha  viongozi wa dini mbalimbali, malengo ni kutaka kuufanya uwe mfuko wa wilaya ambao utawawezesha wanafunzi wote wanaotoka familia duni katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro waweze kunufaika.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari