Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Mtanzania mwenye jinsia mbili aelezea machungu ya kuonekana tofauti katika jamii

“Miaka si mingi sana iliyopita nilizaliwa katika Hospitali ya Amana, Ilala Jijini Dar es Salaaam chini ya uangalizi wa madaktari bingwa wakiongozwa na daktari Peter Wangwe.

Kama ilivyokuwa kawaida kwa wazazi wengine, wazazi wangu pia walikuwa a shauku kubwa ya kujua  jinsia ya malaika mpya waliyemleta duniani.

Lakini, shauku yao iligeuka simanzi na giza nene likatanda; wauguzi waliulizana, wazazi walishangaa na swali likakosa jibu,

“Je? ni wa kike ama wa kiume” Cha kustaajabisha ni kwamba maumbile yangu hayakuafikiana na upande wowote, siyo waliosema wa kiume ama wa kike walikuwa sahihi ….

… Tangu wakati huo mpaka sasa jinsia yangu ina utata,”

“Madaktari walishauri nirudishwe nyumbani na nitaendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi ili kupata muafaka wa utata huo. Muda mchache baadaye nilipelekwa Hospitali ya taifa Muhimbili na kupokelewa na Dkt. Simba ambaye naye alinikabidhi kwa Dkt. Wangwe.

Kwa nafasi zao walipambana kufumbua fumbo hili lakini waliishia kunipa tumaini kwamba pengine kesho, pengine kesho kutwa, labda mtondo ama mtondo goo fumbo lingefumbuliwa. Lakini, miongo imepita sasa na jinsia yangu bado ni tata,”

Hii siyo hadithi ya kufikirika, bali ni ushuhuda halisi wa Baby John Musamba mmoja kati ya watanzania waliozaliwa na wanaoishi na jinsia tata.

Alikuwa akitoa ushuhuda wake katika mkutano uliyowakutanisha watanzania wachache waliozaliwa na changamoto hiyo ya kimaumbile ambao walipata ujasiri wa kujitokeza na kuhudhuria mkutano huo ulioandaliwa na taasisi ya Tanzania Voice of Humanity (TVH) na kuafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Saint Gasper Jijini Dodoma.

Wanasema kazi ya Mungu siku zote haina makosa. Lakini kwa ndugu zetu hawa waliozaliwa na hali hii wanaelezea kukutana na changamoto kubwa katika hatua na nyanja tofautitofauti za maisha yao na shughuli zao za kila siku, ikiwemo unyanyapaa.

Kwa watanzania wengi, swala la  “Jinsi Tata’ bado ni jambo ‘Tata’ kwani ni jambo geni kwa watu wengi ingawa kiualisia wapo watanzania wengi tu ambao wamezaliwa na wanaishi na hali lakini wanakosa ujasiri wa kujitokeza haradhani kwa kuhofia namna hasi ambavyo jamii inaweza kuwachukulia.

Jinsia Tata, (gender ambiguity) ni changamoto ya kimaumbile ambayo mtu anazaliwa akiwa na jinsia zote mbili, yaani, ya kike na kiume.

Japokuwa serikali ya Tanzania imeweka mifumo na sera  nzuri na  rafiki katika kuwatambua, kuwajali na kuwahudumua watanzania wenye aina mbalimbali za ulemavu ili kuhakikisha wanapata huduma stakihi sawasawa na wengine.

Kwa bahati mbaya sana, waathirika wa jinsia tata bado hawajatambuliwa na sera wala mifumo husika iliyowekwa na serikali.

“Tunakutana na changamoto kubwa sana kaika kupata huduma muhimu za kijamii, hususan katika nyanja za elimu, upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na vibali vya kusafiria, zikiwepo Passport na Visa.

Mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu huu akienda kumuandikisha mtoto shule, swali gumu huwa ni ili, ni mwandishe kama wa kiume, ama wa kike?”

Baby Msamba alieleza wakati wa mahojiano maalumu na TAIFA TANZANIA pembeni mwa mwendelezo wa mkutano huo.

 “Watanzania wenzangu hali hii si ya kawaida na imetuchukua muda mrefu sana kujikubali na hatimaye kuchukua hatua ya kujitokeza hadharani.

Fikiria kwa mfano, hapa unaponiona naonekana kama mwanamke mzuri na aliyekamilika, lakini kimsingi mimi si mwanamke,” alisema Baby John Musamba.

Yeye ni mwathirika wa ulemavu wa jinsia mbili ambye ndiye mwanzilishi wa taasisi ya Tanzania Voice of Humanity.

Aliongeza:

“Nimeamua kuanzisha taasisi hii na kujitokeza hadharani siyo kwa ajili ya kupata huruma ya umma (public sympathy), lakini kwa nia njema ya kuisemea jamii ya watu wenye hali hii ya ulemavu wa jinisa tata, wengi ambao hawana ujasiri wa kujitokeza hadharani ingawa wanapitia hali mbaya ya kimaisha kutokana na unyanyapaa,”

MAISHA YA UTOTONI

“Nasikitika kwamba sikuufurahia utoto wangu kama watoto wengine. Kila mara watoto wenzangu walinitenga, hata ndugu, ndugu wa damu nilioamini wangekuwa faraja kwangu pia walinitenga.

Nilikuwa mpweke katikati ya kadamnasi nzima iliyonizunguka.

Hatahivyo, kulikuwa na baba, alikuwepo mama pia, kando ya giza totoro walinipatia mwanga, waliweka nuru mbele yangu nikapata tumaini la kusonga mbele.

Nani kama mama, nani kama baba!!,” Baby Msamba anakumbuka maisha yake magumu ya utotoni.

Siku hazigandi! Anasema kadri muda ulivyozidi kuyoyoma na hatua za ukuaji wa maisha yake zikazidi zikagonga hodi zaidi.

“Mabadiliko ya mwili yalianza kuukaribisha ujana, furaha ya kila mzazi kuona mwanaye akipevuka. Natamani sana nyakati hizo kwangu zingekuja kama zijavyo kwa watoto wengine, walipokuwa wakifurahia kwangu ulikuwa mwanzo wa kilio na majonzi mapya.

Tarumbeta za aina yake zilianza kurindima tena, siyo heri bali shari tupu,” alielezea Baby Msamba, Mtanzania mwenye ujasiri mkubwa.

Anasema, hatua hiyo ikaweka jiwe la msingi la unyanyapaa kwa kuitwa  majina ya ajabu, ambapo kejeli zikawa viitikio kila baada ya sentensi fupi kwa ndefu zilizomzunguka.

“Wengine waliniita dumejike, wengine hili wengine lile,” alieleza.

Kwa mujibu wa Msamba, aliendelea kuitwa majina mengi yasiyokuwa na ‘staha’ na ya ‘kiunyanyapaa mkubwa’ lakini hakujali kwani hakujiumba wala kupenda kuzaliwa na changamoto hiyo japo nafsi yake ilikuwa ikiraruriwa kwa majina hayo makali na  yasiyofaa kutamkwa.

“Muda wote niliwaza, nilifanya kosa gani kuzaliwa? Ama nimefanya kipi kibaya zaidi ya wengine? Kila mara waliipondaponda nafsi yangu na kuizorotesha wakinifanya nipoteze tumaini na kuendelea kutokomea gizani.

Lakini, hata katikati ya bonde la uvuli wa mauti bado kulikuwa na sauti ndogo, iliyojaa upole na tumaini kuu kwamba, ipo siku kilio changu kitasikika, ipo siku maisha yangu yatapata maana tena. Pengine siku hiyo ni leo, watanzania wenzangu mnaposoma makala hii ya mateso ninayoyapitia,”

ELIMU

Katika safari yake ya kupata haki ya msingi ya elimu, Msamba alielezea mambo mazito na magumu sana ambayo alipitia kutokana na changamoto yake ya kimaumbile.

“Kama watoto wengine, nilijiunga na shule ya msingi nikiamini elimu ni ufunguo wa maisha. Nikitumaini kwamba maisha yangu yanaenda kupata ufumbuzi, kwa bahati mbaya nilijikuta katika kitanzi kingine, kila mtu akitamani kufahamu mimi ni wa jinsia gani,” alieleza.

Alisema changamoto kubwa aliyokuwa akikutana nayo ni pamoja na katika matumizi ya huduma za jamii: “Wana wa kike wana sehemu maalumu wana wa kiume vivyo hivyo, lakini hakukuwa na muafaka kwangu mwenye jinsia tata,”alieleza.

Anasema kwa kuamini kuwa mvumilivu hula mbivu, alijipa moyo akijua kwamba hali hiyo pia itapita, na akaamua kuziweka changamoto zote kando na kuzingatia elimu kwa bidii na kwa sababu mtafutaji hachoki, na akichoka keshapata.

“Nilifanikiwa kuhitimu tena kwa ufaulu mzuri sana. Sikujua kwamba kadri nilivyozidi kuongezeka kimo ndivyo ambavyo changamoto zaidi zingenikumba.

Tatizo lililokuwa shuleni likahamia mtaani, jamii yote ikitamani kufahamu muafaka wa suala langu. Nikawa kama mnyama ninayewindwa kila kona sikuwa, wala sina pa kukimbilia,” alisema kwa masikitiko makubwa.

SAFARI YA MATUMAINI

Anasema ujio wa Raisi, Mama Samia Suluhu Hassan katika uongozi ulifufua chemichemi za tumaini jipya ndani yake. Kwa ujasiri aliamua kuanza safari mpya ya kuitafuta thamani ya maisha yake kwa azma thabiti na ya dhati ya kuitumikia jamii ya watanzania ywenye hali kama yake

Hatahivyo, anasema, safari yake ya matumaini ilianza tangu mwaka 2020 ambapo aliamua kupiga hatua na kufanya maamuzi ya kugombea nafasi ya uongoz kwani aliamini moyoni kwamba wakati na majira sahihi kwa yeye kupaza sauti kutetea kundi kubwa la wanyonge, wasiojiweza na waliokata tamaa ulikuwa umefika.

Alisema, aliuona wakati huo kuwa wakati sahihi ambao alipaswa kupaza sauti yangu kwa maslahi mapana ya jamii na taifa lake. “Nilisimama bila kuogopa, mbele nikasonga. Pongezi nyingi kwa baba, mama na familia yangu kwa kunishika mkono na kuniamini,”

Aidha, Msamba ansema alifanikiwa kuzunguka huku na kule akinadi sera zake na kuelezea maono yake kwa uwazi na uthabiti wa moyo akiamini watu wangempima kwa sera bora alizonazo

“Chakustaajabisha, kabla ya kufikia hatua za mwisho za kupiga kura, maswali mengi yaliibuka tena yakihoji juu ya jinsia yangu.

Huzuni ilinijaa nikiihurumia jamii ambayo inafikiria jinsia katika kuchagua na siyo sera. Wengi waliwaza, mtu mwenye ‘jinsia tata’ atawezaje kuondoa ‘utata’ uliopo katika maisha yetu?

Hawakutaka kupima hoja zangu katika mzani wa fikra yakinifu badala yake walidadisi jinsia yangu katika mahakama yao ya bila huruma.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Voice of Humanity Baby Msamba (wapili kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Bodi ya TVH, Lucia Safari (kushoto) wakimkabidhi zawadi ya picha ya spika wa Bunge, Tulia Ackson Mkurugenzi Msaisizi wa kamati za Bunge za utawala na maendeleo ya jamii, Ndg. Gerald Magige (katikati) wakati wa mkutano maalumu ulioandaliwa shirika hilo jijini Dodoma (Picha na Valentine Oforo)

Sintofahamu hizo zikafanya nisiweze kupata nafasi mbele ya wanaume na wanawake. Kwakuwa asiyekubali kushindwa si mshindani, nilikubali matokeo na kumpongeza mgombea mwenza kwa kuchaguliwa lakini pia nikaunga mkono juhudi zake katika kuiendeleza jamii yetu.

Hata hivyo, anasema uthubutu wa kujitokeza hadharani na kugombea uliweka mwanzo mwingine wa safari mpya, kwani katikati ya wengi wasioamini walikuwepo wengine walioamini kwamba anaweza na walikuwa tayari kusimama pamoja naye.

“Hivyo, nikaamua kutafuta njia mbadala ya kupaza sauti ya wanyonge, nikafanya juhudi na kufanikiwa kusajili taasisi isiyo ya kiserikali yenye jina la TANZANIA VOICE OF HUMANITY.

Taasisi hii ina lengo kuu la kupaza sauti kwa jamii kuhusiana na tofauti zetu. Kuijulisha jamii kwamba licha ya jinsia zetu; jinsia ya kike, ya kiume ama jinsia tata, sote ni binadamu na tunastahili nafasi sawa katika kila nyanja ya maendeleo. Jitihada hizi zimefanikiwa kuwafikia watu baadhi katika jamii na kuwaelimisha japo chururu si ndo ndo ndo,” anaeleza.

Licha ya jitihada nzuri alizozifanya za kuvuka ‘misitu na mabonde’ hadi kufikia hatua ya kuanzisha taasisi hiyo, Msamba anasema bado safari ni ndefu na jitihada kubwa sana inahitajika kutoka pande zote.

Serikali na wadau wa sekta binafsi, wanatakiwa kuungana katika kuwasaidia kuinua maelfu ya watoto ambao wanagubikwa na changamoto ya jinsia tata kama aliyonayo yeye.

“Ninatumaini, makala hii itakuwa njia mojawapo ya kuifikia jamii ya watanzania na kwangu mimi, ni jia ya kutoa dukuduku langu la moyoni nikiamini sikio la Raisi, serikali, pamoja na wadau wengine katika maswala ya ustawi wa jamii ni sikivu na kwa uwezo na ushirikiano wao kwa ujumla utasaidia kuinua maelfu ya watoto wenye chagamato ya jinsi tata,” alisema kwa kuamini.

JE! KUNA MATIBABU?

Kwa mujibu wa Daktari Edna Majaliwa, Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto na vichochezi katika Hospitali ya Taifa ya Mhimbili, changamoto ya kwanza ya matibabu kwa waathirika wa jinsi tata ni uhaba wa madaktari waliosomea/bobea katika kutoa tiba kwa kundi la watu wenye changamoto hiyo ya kimaumbile.

“Mpaka sasa, Tanzania ina madaktari wanane pekee wenye ujuzi wa kutoa huduma kwa watu wenye matatizo ya jinsia tata (disorder of sex development -DSD), anaeleza.

Pamoja na upungufu huo, Dkt. Majaliwa anasema wahanga wengi wa ulemavu huo mara nyingi wanashidwa kupata matibabu husika, ikiwemo upasuaji, kutokana na gharama kubwa zinazochajiwa Hospitalini, maranyingi zinaanzia hilini 100,000 hadi 900,000.

Aidha, akielezea zaidi juu ya utaratibu wa matibabu ya waathirika hao, Dkt. Majaliwa anasema:

“ Kulingana na utaratibu wa matibabu ya watu wenye jinsi tata, huwa tunawashari kuja hospitalini wakiwa na umri wa zaidi ya miaka 18 ili waweze kuamua juu ya hali yao ya kijinsia ya siku za usoni, kama watafanyiwa upasuaji, mhusika hapa atapaswa kuchagua jinsia ambayo anataka kubakia nayo, yaani anataka kuwa mwanamume wa kike” alielezea.

“Kimsingi, waathirika wa changamoto ya jinsia mbili (jinsia tata) daima wanapitia hali ambayo kiungo kimoja (jinsia moja) inakuwa na nguvu zaidi ya nyingine, na hivyo kama sehemu ya upasuaji, huwa ni vyema kuiongezea nguvu zaidi jinsia yenye nguvu na kuidhoofisha ile isiyo na nguvu, japo viongo vyote viwili vitaendelea kuwa vilevile,” alifafanua.

IDADI (TAKWIMU) YA WATANZANIA WANAOISHI NA JINSIA MBILI

Kwa bahati mbaya sana, na jambo ambalo linaweza kutumika kuthibitisha kuwa watanzania wanaoishi na aina hii ya ulemavu hawatambuliki, mazoezi ya sensa ya idadai ya watu na makazi yanayofanyika kila baada ya miaka kumi hapa nchini hayajawahi kulitambua kundi hili kama ilivyo kwa watanzania wenye aina nyingine za ulemavu.

Frank Musamba , Mkurugenzi wa fedha na mipango wa taasisi ya Tanzania Voice of Humanity anasema, “Inasikitisha sana kwamba tulijaribu kushawishi uwezekano wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka huu 2022  kujumuisha idadi ya watu wenye matatizo ya kijinsia mbili lakani hatukuweza kupatiwa nafasi hiyo muhimu,” alieleza.

Hata hivyo, kutokana na tafiti walizozifanya, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na takribani watu 9 wanaoishi na jinisa,  ukifwatiwa na mkoa wa Kagera watu 6.

“Kanda ya ziwa inabeba asilimia 30.3 ya watanzania wanaoishi na jinsia mbili wakati asilimia 27 inapatikana katika kanda ya pwani,” alifafanua.

MAOMBI YAKE YA WAZI KWA RAISI SAMIA SULUHU HASSAN

Mpendwa mama! Nakusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama njia ya kuenzi kazi yako njema. Hakika, kazi inaendelea!

Mpendwa mama! Kama ambavyo umekuwa ukijibu vilio vya watanzania, vivyo hivyo ninaamini utajibu kilio changu kwa kuitaarifu Tanzania juu ya uwepo wa jinsia tata, na kuiasa jamii kutukubali jinsi tulivyo maana sisi pia tumezaliwa kama watoto wengine na tunastahili huduma zote kama watu wengine.

Mama, ni ombi langu kwako kutoa nafasi kwa watafiti wa afya wafanye uchunguzi na kuandaa ripoti inayoelezea kinagaubaga juu ya jinsia tata na juu ya uwepo wa watu wenye jinsia tata miongoni mwa watanzania, kwani watoto wenye jinsi tata wanazidi kuzaliwa kila leo.

Baada ya ripoti hiyo kutolewa, napendekeza kwa heshima na taadhima suala hili liingizwe katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya msingi ili kuondoa changamoto ya unyanyapaa kwa watoto walio na jinsi tata.

Aidha, ni maombi yetu kwamba kiundwe kitengo maalumu chini ya Wizara ya Jinsia na Makundi Maalumu kitakachoshughulikia masuala yote ya jinsi tata, kwa kutoa elimu kwa jamii, na kutoa msaada kwa familia ambazo haziwezi kuwatunza watoto wenye changamoto hizo.

Vilevile, vyombo vya habari vishirikishwe katika kutoa elimu na machapisho sahihi yahusuyo jinsi tata yatakayoratibiwa kwa karibu na kitengo hicho katika Wizara.

Mama, hii ni sauti ya mmoja wa watoto wako aliyeko nyikani. Nisingependa kulalama ila uzito wa nira shingoni mwangu unanilazimu nipaze sauti yangu ili nisaidiwe.

Najua, inawezekana nisiwe na nafasi ya kutosha kuelezea hisia za huzuni zilizojaa moyoni lakini kwa uchache huu naomba kwa unyenyekevu mkuu unisikie. Imani yangu sasa ipo kwako. Asante sana mama. Mungu akubariki sana, Mungu aendelee kuibariki Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari