Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Tanzania yaweka saini kituo cha operesheni za Dharura katika Jumuiya ya Maendeleo, Kusini

TANZANIA  limekuwa taifa la kwanza miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu na operesheni za dharura za kanda.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba huo iliyofanyika Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa.

Na hii ni kupitia kamati maalumu ya mawaziri wenye dhamana ya usimamizi wa maafa.

Aliongeza kuwa, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda (SHOC).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, George Simbachawene (aliyekaa) akisaini Mkataba wa Kuanzishwa kwa Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma (kulia) ni Katibu Mkuu Ofisi hiyo Dkt. John Jingu.

Kituo hicho ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji kilizinduliwa  na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Filipe Nyusi mnamo tarehe 21 Juni, 2021.

“Lengo la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya kibinadamu kwa nchi wanachama zitakazokumbwa na maafa,na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa.” alifafanua.

Aliendelea kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi.

Zingine ni kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika tarehe 17 na 18 Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt John Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.

Awali mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo mwanasheria Dkt Phiness Matto, alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri itavyowezekana.

“Natoa Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusaini mkataba huu na tunategemea nchi 11 kusaini mkataba huu” alifafanua Dkt Matto.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari