Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Afrika Kusini yatuma wataalam kujifunza ufugaji Nyuki Tanzania

SERIKALI ya Tanzania imepokea ugeni wa watu 10 kutoka nchini Afrika Kusini waliofika Tanzania kwa lengo la kujifunza juu ya  ufugaji nyuki, hasa kwenye maeneo ya uanzishaji wa manzuki na hifadhi za nyuki.

Ugeni huo, uliowasili mapema jana Jijini Dodoma unajumuisha wataalamu na wafugaji nyuki, ambapo malengo yao pia ni pamoja na kujifunza juu ya maandalizi na ukaguzi wa manzuki pamoja na njia bora za kuzuia na kudhibiti wadudu kwenye ufugaji nyuki.

Akiongea mara baada ya wageni  hao kuwasili,  Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba  amesema ziara hiyo ni ya kimkakati na inalenga kuanzisha mazungumzo na  kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, hususan katika eneo la biashara ya mazao ya nyuki, teknolojia za ufugaji nyuki na utafiti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, kutoka Wizara ya Maliasili na Utali, Deusdedith Bwoyo, amesema  wageni hao  wamehamasika kuja hapa nchini  kujifunza  namna shughuli za ufugaji nyuki zinavyofanyika.

“Kule Afrika Kusini tumeambiwa  wana uwezo wa kuzalisha tani 2000 kwa mwaka wakati asali inayohitajika ni tani 4000 kwa mwaka, Sisi huku tunazalisha tani  32,691  kwa mwaka na asali yote hiyo hutumika kukidhi mahitaji ndani ya nchi kwa takriban asilimia 90 ” amesema Bwoyo.

Pamoja na hayo, Bwoyo ameongeza kuwa, Waafrika Kusini hao wamekuja kujifunza namna bora ambayo itawasaidia kuongeza uzalishaji wa asali nchini kwao, lakini pia,  namna ambavyo wanaweza kuwahamasisha watu nchini kwao kutumia asali kwa wingi kama ambavyo zao hilo la nyuki linatumiwa kwa wingi hapa Tanzania

Naye Kiongozi wa Wajumbe hao ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kilimo na Maendeleo Vijijini Kaskazini Magharibi mwa Afrika Kusini, Zakaria Thupi Mokgathlha, amesema Tanzania ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa kwenye eneo la ufugaji nyuki, hivyo wamekuja kujifunza ili waweze kupata ujuzi utakao wasaidia  kujiimarisha kwenye neo hilo.

“ Tumekuja kuangalia Tanzania inavyofanya kwenye eneo hili ili   tutakavyorudi kwetu  tukaweke mikakati ya kuimarisha sekta hii.” amesema Zakaria.

 Katika ziara hiyo, Wataalamu hao watatembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki kilichopo mkoani Tabora  Uongozi wa Mkoa huo pamoja na Vikundi vya wafuga nyuki vya  mkoa huo.

 Mara baada ya kuwasili Jijini Dodoma, ugeni huo ulipata fursa ya kutembelea Ofisi za Manyoni za  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  pamoja na Hifadhi ya Nyuki ya Agondi  ambapo wamepata elimu ya namna bora ya kufuga na kuchakata mazao ya nyuki hususani asali.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari