Habari, Utamaduni, Historia na Simulizi za Tanzania na Afrika Mashariki

Arusha waanza kuunda Pikipiki zinazotumia Umeme

Chuo cha ufundi Arusha (ATC) imefanikiwa kutengeneza pikipiki yake ya kwanza inayotumia nishati ya umeme ikiwa ni mkakati wa kuachana na matumizi makubwa ya mafuta na utunzaji wa mazingira.

Wataalamu wa chuo hicho kilichopo jijini Arusha wamekuja na ubunifu huo wakati kilio cha uhaba wa mafuta na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ikishika kasi nchini.

Hiyo imesababisha matatizo makubwa katika sekta za usafiri kwa eneo zima la afrika mashariki.

Kenya, Uganda na Tanzania kwa sasa wanatumia usafiri wa pikipiki katika maeneo mengi ya mijini na hata vijijini.

Pikipiki ilitambulishwa rasmi wakati wa ziara ya kamishna wa Elimu nchini Dr. Lyabwene Mtahabwa alipotembelea chuoni hapo ili kujionea ubunifu huo.

Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha, Mussa Chacha alisema kwa teknolojia hiyo mpya itaondoa adha ya uchafuzi wa mazingira hasa hewa ya ukaa inayosababisha ongezeko la joto duniani.

Alisema kuwa mafanikio hayo ni matunda ya mashirikiano baina ya chuo cha ATC na vyuo vikuu vya Seoul university na Hanyang university vya nchini Korea  vyenye lengo la kuanzisha programe ya mitambo inayotumika viwandani.

‘Katika mashirikiano haya, tuliangalia changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo moja ya visababishi ni matumizi makubwa ya mafuta na utatuzi ndio mwanzo wa utafiti huu wa kutengeneza pikipiki inayotumia umeme wa jua na Tanesco”

Alisema kuwa pikipiki hiyo inayochajiwa muda mfupi na kutumika kwa kipindi kirefu.

Pikipiki hizo pia zitakuwa hazitoi sauti au kelele yeyote wakati zitakapokuwa zinatembea.

Baadhi ya pikipiki hizo zimekwishakamilika na sasa chuo kipo mbioni kuzifanyia majaribio ya masafa marefu ya zaidi ya kilomita 100.

Baada kuthibitisha usalama wake wataanza rasmi kutengeneza mazingira ya kuzalisha pikipiki nyingi zaidi kwa ajili ya matumizi kwa jamii.

“Kwa sasa tumeandaa mazingira mazuri ya uzalishaji wa vifaa vya kutengeneza piki piki nyingi zaidi tutakazoingiza sokoni hivi karibuni kwa ajili ya matumizi ya usafiri na biashara”

Akizungumzia piki piki hiyo, Dr. Mtahagwa alisema kuwa serikali inafarijika na matokeo ya chuo cha ufundi Arusha hasa katika ubunifu wa teknolojia mbali mbali yanayojibu changamoto za wananchi lakini yanayoendana na mapinduzi ya nne ya viwanda.

“Piki piki hii inatunza mazingira kwa hali ya juu sana, kwanza haina sauti wala moshi kwani haitumii mafuta ya petrol au dizeli bali umeme wa jua, hakika nawapongeza sana na niwaombe waharakishe uzalishaji wake haraka iwezekanavyo isaidie watanzania wengi zaidi”alisema.

Mmoja wa wataalamu watengenezaji wa pikipiki hiyo, Eng Marchius Tibaijuka alisema kuwa katika utengenezaji wa piki piki hiyo walipitia changamoto mbali mbali ikiwemo baadhi ya teknolojia walizokuwa wanatumia.

“tulianza utafiti mwaka jana na mwaka huu ndani ya miezi nane tumefanikisha na ina uwezo wa kuchajiwa dakika 24 na kutembea umbali wa kilomita 100 bila kuisha hivyo tunaendelea na maboresho madogo madogo iwe rahisi kutumika”

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari