Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Canada yatoa Bilioni 46 Kuwasaidia Wasichana Nchini Tanzania

Serikali ya Canada imetoa jumla ya shilingi billion 45.6 kwa ajili ya kuwainua watoto wa kike wanaokosa fursa za kuendelea na masomo au kujiendeleza kielimu nchini Tanzania.

Ni Mradi maalum kwa ajili ya wasichana wanaoshindwa kumaliza shule wapatiwe mafunzo ya ujuzi na ufundi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa.

Mradi huu unaotekelezwa na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na jumuiya  ya vyuo na Taasisi za ufundi za nchini Canada.

Lengo la msaada huo ni kuboresha ushiriki wa wanawake na wasichana kwenye shughuli za kiuchumi

Akizungumzia mradi huo, mwakilishi wa ubalozi wa Canada, Bronwyn Cruden alisema kuwa serikali yake imetoa jumla ya Dola milioni 25 za Canada ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 45.6 kwa ajili ya kudhamini  mradi huo.

Wasichana wengi Tanzania hukatisha masomo kwa sababu moja au nyingine

Utaendeshwa kwa kipindi cha miaka saba.

Moja ya majukumu yake ni kuwawezesha watoto wa kike kupata Elimu ujuzi lengo ikiwa ni kuwainua kimaisha lakini pia kuongeza viwango vya ushiriki wao katika maswala mbali mbali ya kijamii.

“Tunatambua changamoto wanazopitia watoto watoto wa kike wanapoteleza katika hatua ya kupata Elimu iliyo rasmi, kiukweli inawarudisha nyuma sana ndio maana tumekuja na mpango huu wa kuwawezesha kupata Elimu isiyo rasmi ya ujuzi mbali mbali hasa ufundi na biashara Ili waweze kunyanyuka tena na kuanza maisha mapya hasa baada ya kuelimika na kupata ajira”

Katibu mkuu wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia Dr. Francis Michael

Akifungua mafunzo hayo, Katibu mkuu wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia, Francis Michael amekiri kuwa wamepokea jumla ya billioni 45.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa miaka saba ya kuwainua watoto wa kike walioshindwa kumaliza shule  kwa changamoto mbali mbali.

 “Mradi huu unalenga kuwapatia mafunzo ya ujuzi ambapo tumeshaainisha shule mbali mbali za maendeleo na ufundi kama Veta na tumegawana majukumu ya kuanza kuwakusanya walengwa na kuwaunganisha na vyuo hivyo Kwa ajili ya kuanza mafunzo rasmi”

Alisema kuwa katika mradi huo unafadhili pia zana na vyombo vya kufanyia kazi kama mtaji Ili wanufaika waweze kwenda kujiajiri wanapohitimu Elimu hiyo ya ufundi.

“Tumepokea mradi huu Kwa mikono miwili na tunakwenda kuutendea haki na sisi tutaongeza nguvu zaidi kwani unakwenda sambamba kabisa na malengo na sera ya serikali kumuinua mtoto wa kike aliyekosa fursa ya kupata Elimu,” alisema.

Pia utawapa fursa wasichana kujiunga na kunufaika na mafunzo mbadala ya kujijengea ujuzi kupitia Elimu isiyo rasmi.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari