Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Treni Mpya 10, Mabehewa 270 Kuagizwa ili kukabiliana na wimbi la Safari za Krismas na Mwaka Mpya

treni ya kaskazini ikiwa stesheni ya arusha

Shirika la Reli Tanzania limeanza kuyafanyia matengenezo mabehewa 600 ya mizigo na 37 ya abiria huku likisubiri mabehewa mengine mapya 245 kwa ajili ya mizigo na mengine 22 ya abiria yaliyoagizwa hivi karibuni.

Pamoja na hayo, pia kuna injini au vichwa 10 vipya vya treni vinavyotarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha usafiri wa reli.

Hii ni kwa mujibu wa Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete.

Wakati huo huo shirika la reli limefanikiwa kuvuna zaidi ya shilingi milioni 408 kutokana na huduma za safari za treni kwa kanda ya kaskazini.

Makusanyo hayo ni mapato ya kipindi cha miaka miwili tu za huduma za usafirishaji wa treni ya reli ya kati ya Arusha na Dar-es-salaam kupitia Kilimanjaro.

Usafiri katika reli ya kaskazini ulifufuliwa Novemba 2020 na aliyekuwa Rais wa Tanzania John Magufuli.

Mwakibete amesema kuwa tangu kufufuliwa kwa njia hiyo ya treni imeonyesha mafanikio makubwa katika kuleta mageuzi ya safari za bei nafuu.

“Wananchi wamedhihirishwa na usafiri huu wa treni. Kwa taarifa nilizonazo, abiria wanaotumia njia ya reli wakitokea Dar-es-saalam pekee kuja Arusha ni zaidi ya watu 400.”

“Na tangu kufufua njia hii mwaka 2020 tumeshakusanya zaidi ya shilingi milioni 408 ambazo imeingia kwenye mapato yetu ya ndani…

…Pia tumeweza kusafirisha zaidi ya tani 11600 za mizigo hasa vifaa vya ujenzi kama saruji na nondo pia nafaka kutoka mikoa mbali mbali, ” alisema Mwakibete

Na kutokana na umuhimu na uhitaji wa safari za treni, shirika la reli linaanza kuweka mikakati ya kuboresha huduma za usafiri wa treni zaidi ikiwemo kuongeza njia zingine ili kujenga uwanja mpana wa wananchi kusafiri kwa treni,  sehemu popote nchini.

Alisema kutokana na malengo hayo serikali imeanza ukarabati wa mabehewa 600 ya mizigo, 37 ya abiria huku wakiagiza mabehewa mapya 245 ya mizigo na 22 ya abiria na vichwa 10 Kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha usafiri wa reli nchini.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa uendeshaji wa kanda ya kaskazini, Focus Sahani alisema kuwa usafiri huo umekuwa msaada mkubwa wa kupunguza bei za vifaa vya ujenzi hasa saruji kutoka Tanga na Nondo.

Lakini pia umerahisisha usafirishwaji wa nafaka za mahindi au mchele kutoka maeneo mbalimbali.

Ongezeko kubwa la wateja wanaotumia usafiri wa treni kanda ya kaskazini umelazimisha shirika la reli sasa kuongeza siku moja ya jumatano.

Treni ya kaskazini itakuwa inasafirisha abiria siku tatu za wiki ikiwemo zile za awali za Jumatatu na Ijumaa pamoja na Jumatano iliyoongezeka.

“Watu wa reli tumejipanga kuongeza treni katika mkoa wa Arusha, kwa sababu tarehe 20 tuna ujio wa mabehewa mapya ya treni za kisasa ambazo zitatoa huduma Upande wa Arusha, Kigoma, Mwanza na Katavi, hivyo wateja wetu waendelee kutuamini na kutupa nafasi ya kuwahudumia”

Mkuu wa kituo cha reli Arusha, Victor Ng’ingo alisema kuwa abiria wa kutumia usafiri wa treni wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku na kuwataka wananchi watumie usafiri huo hasa kipindi hiki cha msimu wa sikuu za mwisho wa mwaka kwani hawataongeza bei za nauli.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari