Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

PAPU Tower Jengo refu zaidi Kaskazini mwa Tanzania sasa pia kuwa kivutio cha Utalii nchini

Jengo jipya jijini Arusha, pamoja na kutajwa kuwa ndilo lenye muonekano mzuri zaidi mjini, lakini pia linathibitishwa kuwa ndio mnara mrefu zaidi kujengwa na binadamu kaskazini mwa Tanzania.

Sasa kujulikana kama PAPU Tower, jingo hilo jipya litakalozindulwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 2 Septemba, 2023 limetajwa kuwa ni uwekezaji mwingine wa kimkakati, ambao unaweza pia kutumika kutangaza utalii wa mikutano.

Likiwa na ghorofa 18 pamoja na handaki kubwa chini yake kwa ajili ya maegesho ya magari, jingo la PAPU Tower lipo eneo la Philips, katika kata ya Sekei, likiwa limepakana na Hoteli maarufu ya Mount Meru, mkabala na barabara kuu ya Arusha-Moshi.

Mtu anaposimama katika eneo la juu la jengo hilo anaweza kuyaona maeneo yote ya jiji la Arusha na Viunga vyake.

Ni uwekezaji mkubwa kati ya Umoja wa Posta Afrika au PAPU (Pan-African Postal Union) na serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Ujenzi wa jingo la PAPU umegharimu zaidi ya Bilioni 33, huku asilimia 60 ya hizi, ikitoka katika Umoja wa Posta Afrika na asilimia 40 ikigharamiwa na TCRA.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Selestine Kakele anabainisha kuwa sherehe za uzinduzi wa jingo hilo la kimataifa zitakuwa pia ni kilele cha vikao vya mkutano wa 41 wa utawala wa taasisi za umoja wa posta afrika.

Mkutano huo uliokuwa unafanyika jijini Arusha kwa zaidi ya wiki moja umejumuisha nchi 26 wanachama wa umoja huo.

Inatarajiwa kuwa wakuu wa nchi wapatao watano kutoka nchi mbalimbali, wataungana na Rais Samia Suluhu Hassan katika tukio hilo la uzinduzi wa jingo litakalojumuisha uwakilishi wa nchi 26 Barani Afrika.

Afisa Mtendaji wa Umoja wa Makampuni ya Utalii Tanzania (TATO), Sirili Akko anasema kuwa kwa sababu Jengo la PAPU litakuwa kituo maalum cha biashara, taasisi za fedha, mawasiliano, migawa na pia ofisi za umoja wa Posta Afrika, ni vyema serikali ingeweka mfumo mzuri kwa ajili ya wateja watakaopanga hapo.

Eneo la Sekei lililopo jingo hilo jipya ni sehemu ya biashara mbambali kwa wekezaji wadogo ambao wanaona kuwa uwepo wa mradi huo mkubwa ni fursa nyingine ya kibiashara kwao.

Hata hivyo, waendesha pikipiki za abiria, maarufu kama Boda-Boda wana wasiwasi kwamba pengine watahamishwa kutoka maeneo hayo, pale jingo litakapoanza kutumika rasmi.

Samuel Sarakikya ambaye amekuwa akipaki Pikipiki yake hapo kwa ajili ya kuhudumia wasafiri kwa zaidi ya miaka 15 sasa, anakiri kuwa jengo linaweza kuwa faida kwao iwapo hawataondolewa eneo hilo.

Christopher Mushi dereva wa ‘Tuku-tuk,’ au Pikipiki ya matairi matatu, ziitwazo Bajaji, anabainisha kuwa eneo la PAPU kuna pikipiki 40, Bajaji 6 na Teksi zaidi ya Kumi na kwamba ikiwa wataendelea kufanya shughuli zao hapo, Jengo litakuwa ni chanzo kikuu cha wateja kwao.

Hata hivyo madereva teksi wa eneo hilo wao wana Imani kabisa kuwa huduma zao zitakuwa zinahitajika sana na watumiaji wa jengo jipya hivyo wanasubiri kwa hamu uzinduzi wake.

Lakini hata kabla ya jengo kukamilika tayari vijana wengi walishanufaika nalo kupitia ajira zilizopatikana kipindi cha ujenzi wake.

“Tulikuwa wengi sana hapa, idadi siwezi kutaja na wengi wakiwa ni vijana na wanawake kuanzia kwenye ufundi, vibarua wapishi na wabeba mizigo,” alisema Mohammed Simon ambaye ni fundi umeme wa Prolaty Consult.