Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Hospitali Mpya ya Karatu yakamilika. Itakuwa na Uwezo wa Kuhudumia Wagonjwa 300,000

Hospitali Mpya ya Wilaya ya Karatu kuwahudumia watu zaidi ya laki mbili (Pich na Sophia Fundi)

Hospitali mpya ya wilaya ya Karatu imekamilika hivyo kutimiza ndoto ya siku nyingi miongoni mwa wakazi wengi wa eneo hilo.

Ingawa bado haijazinduliwa rasmi, lakini hospitali hiyo ya kisasa iliyogharimu shilingi bilioni 2.6 tayari imeanza kutoa huduma za matibabu kwa wananchi wa Karatu, Mto wa Mbu, Ngorongoro na maeneo ya Jirani.

Karatu, moja ya wilaya saba zinazounda mkoa wa Arusha, haikuwahi kuwa na hospitali yake yenyewe tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo na pengine tangu Uhuru wa Tanganyika upatikane.

Kwa miaka mingi, wananchi wa wilaya walikuwa wakitegemea kupata huduma za matibabu na ushauri wa afya kutoka hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri iliyopo mjini Karatu.

Zaidi ya watu laki mbili watakuwa wanapata huduma za tiba hospitalini hapo.

Kwa wakazi wengine, walilazimika kufuata matibabu katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru iliyopo jijini Arusha, umbali wa kilometa zipatazo 120 kutoka mjini Karatu.

Wananchi wa maeneo ya mbali na mji ndio walikuwa wakitaabika zaidi maana iliwalazimu kusafiri hadi mjini karatu, halafu tena watafute usafiri kwenda Arusha.

Karatu, ni lango muhimu la utalii wa kaskazini

Akizungumza na wadau mbalimbali wa maendeleo Karatu, Mkuu wa wilaya  hiyo Dadi Kolimba anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa hospitali hiyo ambao ilikuwa ndio hitaji la muda mrefu la wakazi wa Karatu.

Hospitali mpya imeanza kutoa huduma katika baadhi ya majengo huku shughuli za kukamilisha maeneo mengine zikiendelea.

DC Kolimba pia anawashukuru wakazi wa karatu, na wadau wengine mbalimbali walioshiriki kutoa michango ya hali na mali katika kuunga mkono na kufanikisha juhudi za serikali wakati wa ujenzi.

Anabainisha kuwa wengi wao walotoa vifaa mbalimbali na wengine wakiendelea kuchangia.

Hadi sasa, jengo jipya la hospitali bado linahitaji samani na vifaa vingine muhimu vya tiba.

Mganga mkuu wa wilaya ya Karatu, Daktari Lucas Kazingo anasema kuwa ujenzi wa majengo hayo tisa ya hospitali mpya yamegharimu jumla ya shilingi bilioni 2.6.

Kati ya fedha hizo Serikali imechangia Shilingi bilioni 1.6.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) nayo ilitoa kiasi cha shilingi milioni 700 kama mchango wa shirika hilo kupitia mradi wa ujirani mwema.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Karatu, Karia Magaro anaeleza kuwa hospitali mpya sasa imeanza kutoa huduma za afya na tiba katika majengo mawili ya wagonjwa wa nje yaani ‘Out-Patients Department (OPD) na Maabara.

Hii ni kwa sababu majengo mengine bado ya uhitaji wa samani na vifaa vingine muhimu.

DED Magaro ansema kuwa majengo mengine ya hospitali nayo yataanza kutumika kutoa huduma za tiba pale ambapo samani na vifaa vingine vitakavyoendela kupatika.

Mkurugenzi huyo anawaomba wananchi na wadau wengine wanaoguswa na maendeleo ya wilaya hiyo, waendelee kuchangia ili kukamilisha maeneo yaliyobaki, hususan samani na vifaa tiba.

Magaro alisema kuwa hospitali hiyo inatarajia kuwahudumia wagonjwa zaidi ya laki mbili na tisini (290,000), yaani Laki tatu kasoro kumi, wengi wakiwa ni wakazi wa Karatu.

Hata hivyo kwa sababu Karatu pia ni lango la utalii kwa wageni waendao Serengeti na Ngorongoro, vile vile wasafiri wanaoelekea Musoma, hospitali inatarajiwa kutoa huduma za afya kwa wakazi na wageni wengine kutoka maeneo mbalimbali ya Arusha, Kanda ya Ziwa na Wasafiri.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari