Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Lambert Dorr: Padre Kutoka Ujerumani Aliyeacha Historia ya Ajabu Ruvuma

Eneo la Peramiho moani Ruvuma, ni eneo lenye kumbukumbu nyingi muhimu zinazostahili kutunzwa zaidi hasa kwa maandishi.

Na kati ya watu muhimu waliopitia Peramiho ni pamoja na Padre Lambert Dorr.

Padre Dorr pengine ndiye Mjerumani aliyeipenda zaidi Tanzania kuliko Ujerumani yenyewe.

Na si ajabu aliipenda Tanzania kuliko watanzania wengi wanavyoweza kuipenda nchi yao.

Kwake yeye lugha ya Kiswahili haikuwa tatizo kabisa. Aliimudu vema.

Padre Lambert Dorr alizaliwa mwaka 1936 katika kijiji cha Gerolzahn kwenye jimbo la Freiburg huko nchini Ujermani.

Mwaka 1956 alifanikiwa kufunga nadhiri za muda baada ya kuaminiwa utawani.

Ameishi Afrika kwa muda mrefu pengine hata kuliko muda alioishi Ujerumani.

Alikuja Afrika Mashariki na kuanza maisha Peramiho ambapo tayari wenzao walishatangulia na kuweka makazi Pugu kisha Peramiho na maeneo mengine Tanzania, Kenya na Uganda.

Alifunga nadhiri za Utawa mwaka 1956.

Baadae akapata nafasi ya kuwa padre. Lambert alikuwa mtaalamu wa Historia. Amefundisha katika maeneo mbalimbali Tanzania ikiwemo Kigonsera.

Mahali alipofundisha kwa muda mrefu ni Peramiho ambapo walimpa jina la utani kuwa ni “WALKING ENCYCLOPEDIA” kutokana na kichwa chake kiwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu nyingi za kitaaluma na zisizo za kitaaluma.

Aliteuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Abasia ya Peramiho, nafasi ambayo ameihidumu kwa miaka 30 kwa mafanikio. Moja kati ya mambo aliyofanikiwa ni kuvunja utengano.

Ni kama alivunja “Apartheid” fulani, ni pale aliporuhusu Waafrika nao kujiunga na utawa badala ya Wazungu pekee.

Haikuwa kazi rahisi kwa wazungu kuchangamana na Waafrika katika uga huo lakini yeye aliwafunza kuwa kitu kimoja kwa amani na upendo.

Na leo tunao Watawa wengi wa kiume hapa Tanzania waliopita mikononi mwa Lambert Dorr.

Huenda wenzake walishangaa lakini aliona kwamba itafika wakati wazungu na Waafrika watapaswa kuchangamana na kufanya kazi pamoja bila kubaguana.

Na hivyo akawapa fursa Waafrika kujiunga na Utawa ambapo walipatiwa elimu husika na kwa weledi.

Katika maisha yake amefanya mengi mazuri na makubwa.

Awali alipanga kuwa akifa azikwe Tanzania na siyo Ujerumani.

Lakini kutokana na kusumbuliwa na mguu wake wa kushoto mara kwa mara, madaktari walimshauri aende nyumbani kwao Ujerumani kwa matibabu zaidi.

Si rahisi kueleza yote hapa kwani ni mengi na wasifu wake kwa ujumla unahitaji maelezo marefu zaidi.

Katika uongozi wake wa Abasia ya Peramiho amejitahidi kushirikiana na wenzake waliokuwako Kenya na Uganda katika kusaidia watu mbalimbali wenye shida mbalimbali hasa yatima na wengine wengi.

Alirudi nyumbani kwao Ujerumani mwaka 2015.

Ni baada ya kuishi Afrika kwa muda mrefu.

Kutokana na hali yake kiafya, alipelekwa katika nyumba ya wagonjwa kwenye Monesteri ya Muncherschwarzach kwa ajili ya matibabu zaidi.

Na Tarehe 22 Oktoba mwaka 2017 alifariki dunia.

Ameacha historia nzuri eneo la Peramiho, nchini Tanzania.

Habari Zingine
Tuachie majibu

Anwani yako ya Email haitaonekana