Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Tatizo la Kukatika Daraja la Zira Mkoani Songwe limekwisha rasmi

Wakala wa Barabara nchini imefanikiwa kutatua tatizo la muda mrefu la kukatika kwa barabara eneo la Zira Barabara ya kutoka Chang’ombe hadi Patamela yenye urefu wa Kilometa 55.7 baada ya kujenga miundombinu imara na ya kudumu katika eneo hilo korofi mkoani Songwe.

Eneo hilo la Zira kwa muda mrefu limekuwa korofi kwa kuadhirika na mafuriko ambapo barabara ilikuwa haipitiki kabisa hasa kipindi cha mvua kiasi cha kupelekea watumiaji wa barabara hiyo kuvuka kwa kutumia Mitumbwi baada ya vyombo vya moto kushindwa kupita na hivyo kusababisha adha kubwa kwa Wananchi.

Akizungumzia barabara hiyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barababa katika mkoa wa Songwe Mhandisi Suleiman Bishanga amesema barabara hiyo ni muhimu kwa sababu inaunganisha mkoa huo na Mbeya kuelekea Tabora kwa upande wa Makongolosi na Singida na kwamba ana imani na Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasaan mtandao wote wa barabara hiyo utaendelea kujengwa na kuboreshwa.

Naye Kaimu mkuu miradi ya Maendeleo wa wakala wa barabara, Songwe Joseph Homviye amesema ili kumaliza kabisa tatizo Serikali kupitia wakala wa barabara imechukua hatua ya kuimarisha tuta kwa kuongeza tabaka za changarawe na kuweka mabox Kalvati makubwa saba ambayo yanasababisha maji kupita vizuri na kupelekea barabara hiyo ipitike vizuri muda wote wa majira yote ya mwaka.

Kwa upande wake Mhandisi Kajashi Njelembi kutoka kampuni ya GNMS Contractors inayojenga kipande cha barabara hiyo amesema kazi kubwa iliyofanyika katika eneo hilo ni ujenzi wa Kalvati kubwa na kunyanyua tuta kwenye kiwango ambacho maji hayawezi kuvuka barabara.

“TANROADS iliweka fedha na sisi tumefanya kazi, mpaka sasa tumeshaweka matabaka 6 ya kiwango cha changarawe katika kipande cha Kilometa 3.6, kazi nyingine zitaendelea ikiwemo kuweka Kalvati ndogo ndogo 5 ili kukamilisha kipande chote kilichokuwa na changamoto ya maji kusomba barabara, mpaka sasa ujenzi umefikia Asilimia 98.

Mradi ulipangwa kukamilika, kabla ya tarehe 25 mei 2023 ambapo kazi zote zingekuwa zimekamilika kwa ubora na kiwango ambacho kinatakiwa” ameongeza Eng: Kabashi Njelembi.