Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mfugaji amlabua Risasi Mkulima Simanjiro

PAUL Laizer ambaye ni mfugaji wa jamii ya kimasai, anashikiliwa na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Manyara kwa tuhuma za kumshambulia kwa risasi, Walter Kaaya ambaye ni mkulima.

Tukio hilo limeripotiwa katika Kata ya Loobosaiti, Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara wakati Kaaya mwenye umri wa miaka 34 alipokuwa akiitoa mifugo ya Laizer (43) inayodaiwa kuingizwa ndani ya shamba lake.

Dada wa majeruhi, Glory Kaaya amesema, mfugaji Laizer alimshambuliwa kwa risasi kaka yake Kaaya kisha akakimbilia kusikojulikana.

Baadae mtuhumiwa alikutwa nyumbani kwa mganga wa kienyeji akiwa katika harakati za kujizindika kwa madawa asili.

Kamanda wa Polisi Mkoani wa Manyara, George Katabazi amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kamanda Katabazi ameonya wananchi wanaomiliki silaha kuacha kuzitumia vibaya kwa kueleza kuwa matumizi mabaya ya silaha ni kuvunja sheria na pia aliwataka wananchi wanaomiliki silaha katika mkoa huo kuzingatia matumizi yake.

Glory Kaaya amesema kaka yake amelazwa chumba cha wagonjwa mahututi wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro (KCMC) mjini Moshi.

“Risasi ilimpiga kifuani upande wa kulia na tunaambiwa na matabibu kuwa imeharibu huko ndani na hivi sasa mapafu yake yanatoa maji mara kwa mara kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata,” amesema Glory.

Amesema tayari madaktari wameshamfanyia upasuaji lakini bado tatizo la kutoka maji kwenye mapafu halijaisha na kwamba kila siku madaktari wanamtoa maji kwenye mapafu.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wakati mkulima huyo akitoa mifugo ya Laizer kwenye shamba lake lenye mazao mchanganyiko, Lazier alitokea vichakani ghafla na kumpiga risasi.

“Tunaomba serikali iingilie kati hii migogoro baina ya wafugaji na wakulima.”

“Sisi wakulima tunaotesha mazao yetu lakini wenzetu wafugaji hawathamini gharama tunazotumia na badala yake wanaingiza mifugo yao kwenye mashamba yetu na kuharibu mazao yetu,” amesema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Kwa upande wake, Kamanda Katabazi amesema Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa za kutokea kwa shambulio hilo, lilianza kumtafuta mtuhumiwa aliyekuwa amekimbia na lilimkamata akiwa eneo la Ziwa la Nyumba ya Mungu alikokuwa amejificha.

“Wananchi walifikiri kwamba kwa kuwa mtuhumiwa ni mtu mwenye mifugo na fedha ni vigumu kukamatika, lakini sisi Jeshi la Polisi kwa weledi na maadili tulimkamata na kumtia mbaroni na sasa tunafanya utaratibu wa kumfikisha mahakamanim,” amesema Kamanda Katabazi.