Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mtoto wa Donald Trump atua nchini Tanzania

Donald Trump Junior ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump amewasili nchini Tanzania kwa kile kinachoelezwa kuwa ni ziara binafsi ya kitalii.

Trump Junior ndiye Mtoto wa kwanza wa Rais wa 45 wa Marekani, aliyetawala taifa hilo kubwa kwa kipindi kimoja.

Mara tu baada ya kutua nchini, Donald Trump Junior alifanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa jijini Dar-es-salaam.

Katika mazungumzo hayo ya kawaida, Waiziri Mchengerwa amemkaribisha Trump Junior kuja kuwekeza nchini katika maeneo kadhaa yanayohusika na sekta ya usafiri, utalii, hoteli na uhifadhi.

Donald Trump Junior in mfanyabiasha mkubwa sana nchini Marekani na ndiye msimamizi wa shughuli zote za uwekezaji za baba yake.

Lakini pia, yeye na mdogo wake Eric Trump wanamiliki vitalu vya uwindaji katika maeneo kadhaa ya nje ya jiji la New York.

Trump Junior ameelezea kufurahishwa na nchi ya Tanzania na kwamba angependa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa ya kanda ya kaskazini.

Donald Trump Junior ni mwandishi wa vitabu, pia hufanya vipindi vya Televisheni na vile vile hujihusisha na masula ya harakati za kisiasa.

Hata hivyo, yeye hasa amesomea masuala ya Uchumi.

Mtoto huyo wa rais mstaafu wa Marekani ni maarufu sana katika mitandao ya kijamii akiwa na wafuatiliaji zaidi ya Milioni 20 katika majukwaa ya Twitter, Facebook na Instagram.