Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Mikaeli Ahho: Chifu Mkatili Zaidi kuwahi kutokea katika Jamii za Wairaqw

ofisi ya halmashauri ya mji wa mbulu

Historia ya Chifu Mikaeli Ahho, ni adimu kama ilivyo picha yake ambayo kwa kweli haipatikani.

Hata hivyo hii ifuatayo hapa inatokana na kuunganisha baadhi ya Mapokeo na Maandiko ya kale.

Inaaminika kuwa Chifu Mikaeli Ahho alizaliwa Miaka ya 1880s

Mikaeli Ahho Alisoma katika shule za kimisionari.

Swala la Utawala wa Kichifu katika Ardhi ya Wairaqw lililetwa na Serikali ya Kikoloni, kabla ya hapo wairaqw hatukuwa na mfumo huu wa kitawala wa Kichifu.

Mwaka 1925 Mikaeli Ahho akiwa kama Mkristu Mkatoliki aliteuliwa Kuwa Chifu wa Juu kabisa wa Mbulu  na Alikuwa Chifu wa Kwanza Kuelimika, na aliyeongoza kwa muda mrefu

Vile Vile Chifu Ahho alikuwa Chifu wa Kwanza kuteuliwa na Serikali ya Kikoloni ya Waingereza

na Kuanzia mwaka 1931 akawa kama Kiongozi wa Hazina wa Kabila la wairaqw na Mbulu kwa Ujumla, Serikali ya Kikoloni ilimtumia kwa maswala ya ushauri na alipata mamlaka ya kutunga sheria ndongo ndogo zitakazotumika katika Mahakama ya Mwanzo.

Ahho alitumia adhabu za kikoplo kuwaadhibu watu ili aweze kukubalika na kuheshimika na kutiiwa kwa jamii ili kuthibitisha mamlaka Madaraka yake, adhabu hii ilianzishwa na serikali ya Kikoloni ya Wajerumani na Ahho alirithi hizo adhabu toka kwao.

Wazee wanasema kwamba utozaji wa Kodi au Ushuru wa serikali kupitia Ahho ulikuwa Utozaji Mbaya Mno kuwahi kutokea, walimwita jina la “Mangi” na hata “Mbwa” kwa sababu watu hawakumpenda Ahho.

Alijifanya kama Rais na Mtu ambaye hakutii amri ya Ahho alipigwa Viboko 25, na kwa Maana hiyo alifanikisha kirahisi mno utawala wa Serikali ya Kikoloni, na waingereza walimchukulia Ahho kama Kiongozi mwenye Akili na Nguvu.

Pia serikali ya Kikoloni ilimpa Mamlaka makubwa Ahho, alikuwa kiongozi wa wa-Jumbe Wote na viongozi wengine wa Falme ya Kiiraqw na kodi zote walizileta kwake na yeye ndiye aliyewalipa Mishahara

Pia Chifu wa Wairaqw (Ahho) alikuwa akifanya kikao mara moja kwa mwezi na Chifu wa waDatoga kutatua Changamoto Mbalimbali zilizokuwa zikiikabili wilaya na Jamii yao kwa Ujumla pia waliunda mahakama ndogo.

Mwaka 1930 Mgogoro wa kimamlaka ulizuka kati ya Ahho na Manda-Do-Bayo.

Manda walimtaka Ahho ajiuzulu na kutimiza azma yao wakatuma Barua ya Malalamishi kwenye Ofisi ya utawala wa serikali ya Kikoloni ya Waingereza iliyopo Arusha.

Baada ya hapo mawasiliano kupitia barua yalifanyika kati ya serikali ya wilaya na ya mkoa kutatua swala hilo, hata na hivyo ofisa wa wilaya alimchagua Ahho kwa Kishindo akidai Ahho ni mwiraqw Kamili (Pure Iraqw).

Yaani ni tofauti na Manda ambao wanaaminika ni wageni katika Ukoo wa Kiiraqw pia Ofisa huyo aliwashutumu manda kuwa wana Uchu wa Madaraka na wana tamaa ya Mamlaka. 

Aliongeza kuwa Ukoo wa Manda haufai kuwa Viongozi wa Kabila hilo na Hilo hajapanga yeye na Ofisi yake Bali Wairaqw hawataki Kuongozwa na Manda. 

Kisha Ofisa huyo Akanukuu maneno ya Kiongozi wa Upande wa Manda aliyesema

“Hii Nchi (Mbulu) ni yetu na tutaitawala.. Watu watake au wasitake na hakuna kitakachotuzuia!”

Hata na Hivyo Sapoti Kubwa ya Afisa wa Wilaya bwana L.S Gruning ilisaidia kumpa Mamlaka tena Mikaeli Ahho Hivyo kuwashinda tena Manda do Bayo.

Zamani Ukeketaji wa Wanawake “Marmo” ilikuwa ni Mila Muhimu Mno kwa Wairaqw na ilikuwa ikifanywa tu na ukoo wa Manda do Bayo na watu wa Ukoo Huo walikuwa wakilipwa ada kubwa kwa ajili ya Kufanya tukio hilo la Kimila

Mwaka 1930 Michaeli Ahho alikataza Rasmi ukeketaji wa wanawake ”Marmo” hii ni kutokana na yeye kuwa na ushindani wa kimamlaka na Manda do hhay Bayo.

Hasa Kiongozi wao Nade Be-a, Ahho alifanikisha hili kwa kuwa alikuwa na sapoti kubwa ya Serikali ya Kikoloni, inaaminika Ahho alikuwa na Mamlaka Makubwa sana na Kujiona yupo juu ya hhay manda do bayo.. 

Inaaminika kuwa ”Nade Be-a alikuwa akitoza faini na ada kubwa kabla ya kutoa ruhusa au Baraka na madawa kwa kwa ajili ya kukeketa (Marmo), 

Basi ikatokea siku wakamchukua Binti wa Ahho kumfanyia hiyo tohara na zamu yake ilipofika Ahho alikataa kutoa ada ya kufanyiwa tohara binti yake.

Kisha kwa msaada wa askari wa kikoloni akawatoa mabinti wote na kisha kuwarudisha makwao japo kwa wakati huo hao mabinti hawakuonekana kama wamekamilika kuwa wanawake hivyo hawakuwa wakishirikishwa katika Shughuli za Maendeleo.

Na pia kushindwa kuwahoji wanaume katika ugawaji wa Ardhi na Miradi Mingine ya Kimaendeleo

Na hapo ndipo Ahho alipotoa Onyo kali kuwa atakayefanya hilo tukio kutakuwa na faini Kubwa Mno. Kisha utamaduni huo wa tohara kwa wanawake ukaishia hapo.

Japo inaaminika kwamba Baada ya Ahho kukataza kisheria kufanyika kwa “Marmo” unaambiwa Wairaqw waliifanya Hii mila kwa siri sana

Japokuwa Ahho yeye mwenyewe alidai Kwamba alikataza Mila hiyo kwa sababu Mwanamke aliyempenda Alikufa kwa sababu ya kufanyiw tohara.

Pia Wakati wa utawala wa Ahho Ulitokea Mgawanyo wa Ardhi uliokuwa ukifanywa na serikali ya Kikoloni.

Chifu Mikaeli Ahho akaiambia serikali ya Kikoloni kuwa Maeneo ya Upande wa Kaskazini mwa Mbulu (kwa sasa ni Karatu) kuwa ni ya wairaqw.

Kuhusu hili serikali ikamtaka athibitishe uhalali wa Ardhi hiyo kuwa ya Wairaqw, baada ya kusikia hivyo Ahho unaambiwa alijaza Gari na Mawe (Tlaa) yale ya Kusagia Mahindi na Kisha kwenda Kuyachimbia maeneo hayo.

Baada ya kuulizwa tena Ahho hakujibu kitu akamchukua bwana shamba wa serikali na kumpelea maeneo aliyochimba yale mawe na na kumuonesha jiwe baada ya jiwe kumueleza kuwa kila mtu anajua wamasai hawalimi mazao ya chakula na haya mawe ya kusagia sio ya kwao.

Akawaambia kwa maana hii, hii ardhi zamani ilikuwa ni ya Wairaqw Kabla ya Kunyang’anywa na Wamasai.. kwa ushahidi Murua wa Ahho serikali ya Kikoloni ilikabidhi Ardhi hiyo Mikononi mwa Wairaqw.

Mwaka 1935 mgogoro wa maji katika Mto Ndero ulitokea kati ya wairaqw, wadatoga dhidhi ya Mmiliki wa mashamba ya Oldeani (nadhani John Unter).

Mjerumani huyu alitumia maji ya mto huu kumwagilia shamba lake la kahawa kitu kilichosababisha uhaba wa maji kwa mifugo ya wairaqw na wadatoga.

Hiyo ilimfanya Chifu Ahho achukue hatua madhubuti akishirikiana na ofisa wa wilaya na kumpa sharti bwana Unter kuwa asinyeshee shamba lake kabla ya saa moja asubuhi na Mwisho iwe saa kumi jioni.

Baada ya Kuona hiyo Mbinu imefeli kwani maji bado hayakutosha ni bwana Ahho aliyeleta wazo la Kujenga Bwawa la Zege (Concrete Dam) ili Kuhifadhi Maji Hayo kwa gharama za wananchi, Waingereza walimkubali sana na Kumuona mtu mwenye Akili sana.

Kihistoria Wakatoliki walimpenda Ahho kwa sababu alikuwa ni Mkristu na hii ilimsaidia kukuza jina lake kwani kanisa Hilo lilikuwa Limeungana vyema na Serikali ya Kikoloni,   na kuwashinda ukoo wa Manda ambao ulikuwa ni wa Kiganga

Pia Alikuwa Muasisi wa Sheria za Wairaqw zilizoanzishwa mwaka 1930

Mikaeli Ahho Alifariki Mwaka 1935, Baada ya Kifo chake Manda do Hhay Bayo wakawa na Mamlaka Makubwa ndani ya Kabila la Wairaqw.

Bwana Winter anasema kwamba Manda do Bayo walijaribu kuushawishi utawala wa serikali ya Kikoloni ili Chifu Mwenye Madaraka Makubwa na Jumbe wote wawe wanatoka katika Ukoo wa Manda.

Nimeandika Historia Hii kwa Kuunganisha Vyanzo mbalimbali, Pengine Kuna mengine ambayo sijayaandika Hapa, Kama una sahihisho au Nyongeza tafadhali tuwekee kupitia sehemu ya Maoni. 

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari