Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Ng’ombe zaidi ya 15 wafa Monduli baada ya kula majani yenye sumu

Ng’ombe zaidi ya 15 wamekufa baada ya kula majani yanayosadikiwa kuwa na sumu katika kijiji cha Losirwa, kilichopo kwenye kata ya Selela, wilayani Monduli mkoani Arusha.

Taarifa za awali zinasema kuwa Mifugo hiyo, imekutwa imekufa katika maeneo ambayo majani mpya yamechipua kufuatia mvua chache zilizoanza kunyeesha maeneo mbalimbali ya Kanda ya Kaskazini.

Kufuatia mvua hizo za vuli majani mapya yameanza kuota katika maeneo kadhaa yatumikayo kama malisho katika kijiji hicho cha Losirwa na pia kwenye Kata nzima ya Selela wilayani Monduli.

Mkuu wa wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe  amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo vya hasa ngombe na wanyama wengine.

Kwa mujibu wa Mwaisumbe hadi muda huu zaidi ya Ng’ombe 15 walikuwa wamekwisha kufa katika maeneo kadhaa wilayani humo.

Uchunguzi kuhusu majani yanayodaiwa kuwa na sumu, bado unaendelea na taarifa husika zitatolewa baadae.

Baadhi ya wafugaji wa wilaya ya Monduli wamesema kuwa kawaida Majani ambayo huchipua kutokana na mvua zinazonyeesha baada ya kipindi kirefu cha ukame huwa na madhara kwa ng’ombe na mifugo mingine.

Wakati huo huo, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Monduli imeagiza mizoga ya mifugo iliyokufa kwa kula majani hayo, ifukiwe mara moja.

“Nimepata taarifa za mifugo kufa kutokana na majani hayo na sasa tumeagiza ifukiwe ili watu wasile m mizoga yake kwani ni sumu” anaeleza Mwaisumbe.

Amesema zoezi la kufukiwa mifugo ambayo imekufa linasimamiwa na polisi ili kuhakikisha hakuna watu ambao watajaribu kuichukua na kupeleka majumbani kwa ajili ya chakula.

Mmoja wa wafugaji ambao mifugo yao imekumbwa na madhara hayo ni Lememo Mollel.

Mollel anakiri kuwa Ng’ombe zake wamekufa mara tu baada ya kula majani ambayo yameota kutokana na mvua za kwanza kunyesha baada ya ukame.

“Hii sio mara ya kwanza, mifugo kufa kila baada ya ukame kutokea mvua zikianza kunyesha majani yenye sumu huota na mifugo wakila hayo majani huwa wanakufa.” amesema

Hata hivyo, aliomba Serikali kusaidia upatikanaji wa  malisho ya mifugo hasa kipindi hiki cha Ukame.

Daktari wa Mifugo kutoka shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Moses Ole-Neselle amesema kufa mifugo kunatokana na kula majani mabichi ambayo yanasumu kutokana na kutokamaa.

“Mifugo inakufa pia kwa sababu bado utumbo haujazoea kula majani machanga na mabichi ambayo huota kufuatia mvua za awali na ambayo huwa hayajakomaa,”

Aliongeza kuwa wanyama wengi kwanza huwa wanaharisha na wengine kufa kabisa.