Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Tanzania yaanza kutoa mafunzo ya Nishati Safi Kwa Nchi za Afrika Mashariki

Kituo cha Kikuletwa

Zaidi ya vijana 200 wa Kitanzania wameanza kozi za mafunzo maalum ya nishati katika kituo cha kufua umeme kilichopo eneo laKikuletwa, katika wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.

Wakati huo huo chuo hicho cha nishati jadidifu cha Kilimanjaro kinajiandaa kupokea wanafunzi wengine kutoka Kenya, Ethiopia na nchi zingine za Afrika Mashariki.

Kituo hicho cha kikuletwa kinaendeshwa na Chuo Cha Ufundi cha Arusha (Techinical College) yaani ATC na kimeanza na mafunzo katika ngazi za ‘Artisans,’ and ‘Technicians.’

Chuo cha Kikuletwa ni miongoni mwa taasisi zilizopo chini ya mradi maalum wa Mafunzo ya Umahiri katika ujuzi uletao mabadiliko kupitia ushirikiano wa kikanda katika eneo la Afrika Mashariki yaani East Africa Skills for Transformation and Regional Integration (EASTRIP).

Mradi huu maalum wa ukufunzi  unajumuisha nchi za Kenya, Ethiopia na Tanzania.

Msimamizi wa mradi huo nchini, Sithole Mwakatage anasema kuwa Benki ya Dunia imewekeza zaidi ya Dola million 16 kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha umahiri wa nishati jadidifu cha Kikuletwa.

Fedha hizo zimeekezwa katika upande wa ujenzi na ukarabati wa majengo, ununuzi wa vifaa na kuwajengea uwezo wakufunzi.

Tayari wanafunzi zaidi ya 200 wa awali kutoka Tanzania wanapata elimu ya nishati jadidifu za umeme yaani umeme wa jua (Solar Energy), Nishati ya Upepo (Wind energy) na nishati inayotokana na mimea, gesi asilia pamoja na mboji, yaani Bio energy.

Mkurugenzi mkazi wa bank ya Dunia nchi za Malawi, Tanzania, Zambia na Zimbabwe Nathan Belete ambaye ni raia wa Ethiopia amefanya ziara katika Chuo Cha Ufundi Arusha kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Baadhi ya Majengo katika Chuo cha Kikuletwa

Belete alipata fursa ya kukutana na wanafunzi wanaosoma masomo ya uzalishaji nishati jadidifu (renewable energy) pamoja na kutembelea karakana na maabara za mafunzo chuoni hapo.

“Nimeridhishwa na gharama ndogo zilizotumika kwenye ujenzi wa miradi hii mikubwa yenye tija.”

“Naahidi kuwa Benki ya Dunia itaendelea kugharamia mafunzo kama haya kwa vijana barani Afrika ambao wanajengeewa uwezo wa kujiajiri,” alisema Belete

Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Arusha Daktari Musa Chacha, anasema kuwa ni bahati ya kipekee kwa ATC kutembelewa na Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia.

“Hii ni kwa sababu Mkurugenzi ameteuliwa Mwishoni mwa Mwezi Oktoba, 2022 na hivyo basi ziara yake ya kwanza kabisa ameifanya hapa chuoni kwetu Arusha.”

Kwa mujibu wa Dokta Chacha, ujio huo ni heshima kubwa kwa Chuo Cha Ufundi Arusha.

“Hii ni taasisi yake yakwanza  ya elimu kuitembelea tangu aanze kazi na hii itafungua milango kwa taasisi zingine kuwekeza katika chuo cha ufundi Arusha” alisema Mkuu wa Chuo.

Hivi sasa kuna mkakati mkubwa ulimwenguni wa kuhamia kwenye vyanzo safi vya nishati ya umeme, ikiwemo vyanzo vya upepo, jua au maji, katika harakati za kuhifadhi mazingira na kupambana na ongezeko la joto duniani.

Sekta ya nishati jadidifu inazidi kustawi duniani kote na vyanzo vya nishati jadidifu vimekuwa ni biashara kubwa duniani.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari