Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

‘Wafungwa wasilazimishwe Kupima Ukimwi!’ Mahakama Yaamuru

Dar es Salaam.

Mahakama Kuu imesema kitendo cha maofisa wa magereza kuwalazimisha wafungwa kupima Virusi vya Ukimwi (VVU) bila ridhaa yao na kutangaza majibu ya vipimo vyao hadharani ni kinyume cha sheria.

Majaji, Elinaza Luvanda, Edwin Kakolaki na Sedekia Kisanya wamekubaliana na ombi la kikatiba lililofunguliwa na wabunge wa zamani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi na Peter Msigwa.

Wabunge hao wa upinzania wamedai kuwa kuwapima wafungwa Ukimwi bila ridhaa yao kunakiuka utu, haki ya faragha na uhuru unaolindwa na Ibara ya 12 (2) na 16 (1) ya Katiba.

Uamuzi wa mahakama unatokana na ombi la kikatiba lililofunguliwa mwaka 2020 na wanasiasa hao dhidi ya Kamishna Mkuu wa Magereza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wanasiasa hao wakipinga vifungu kadhaa vya Sheria ya Magereza walivyodai vinapingana na Katiba na kukiuka haki za wafungwa.

Moja ya mambo waliyoyapinga ni utaratibu wa magereza kuwalazimisha wafungwa wanaoingia gerezani baada ya kuhukumiwa, kupima virusi vya Ukimwi bila ridhaa yao na majibu ya vipimo kutangazwa hadharani.

Wanasiasa hao pia walikuwa wakipinga utaratibu wa magereza wa kupanga muda na mara ngapi mfungwa anaweza kutumia na kubaki sehemu za kujisaidia, utaratibu wa kuwapekua kwa kuwavua nguo na kuwaacha watupu mbele ya wenzao.

Wanasiasa hao machachari ambao kwa nyakati tofauti wamewahi kuonja adha ya jela, walilalamikia pia wafungwa kupewa sare moja bila mbadala, kufurika kwa magereza na uhaba wa vifaa vya kulalia na kuwafanyisha kazi wafungwa bila malipo.

Walilalamikia pia vitendo wanavyofanyiwa wale waliotengwa, kuzuia ndugu kuwatembelea, utoaji wa chakula na mlo chini ya kiwango kinachotakiwa, nguvu ya kisheria wanayopewa maofisa magereza kuwaadhibu wafungwa kwa makosa wanayotenda wakiwa magereza na adhabu ya viboko inayotolewa na maofisa magereza.

“Hakuna sheria yoyote inayoruhusu upimaji wa lazima wa Ukimwi kwa wafungwa, kwa hiyo, haiwezi kusemwa kitendo hicho kinaruhusiwa na sheria.

“Kwa ufupi, vitendo vya kuwalazimisha wafungwa kupima virusi vya Ukimwi na kutoa majibu yao kwa watu wasiohusika, hakiungwi mkono na sheria yoyote, kwa hiyo kinakiuka haki ya utu ya wafungwa, haki ya faragha na uhuru unaotolewa na Ibara ya 12 (2) na 16 (1) ya Katiba,” walisema majaji hao.

Maneno ya Msemaji wa Magereza, SSP Amina Kavirondo, aliyowahi kuyatoa katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu upimaji virusi kwa wafungwa yalikuwa sehemu ya ushahidi wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo.

SSP Amina alisema upimaji virusi vya Ukimwi kwa wafungwa ulifanywa pindi wanapopokelewa na siku wanapoachiwa na kwamba hilo lilifanywa kwa nia njema ili kuhakikisha wafungwa wanahudumiwa kulingana na hali zao za kiafya.

Hata hivyo, majaji hawakukubaliana na hoja hiyo; “Hatuna shaka kwamba utaratibu huo unaweza kufanyika kwa nia njema pale unapoendana na viwango vya utaratibu vinavyokubalika.

“Hata hivyo, kila jambo linalofanyika lazima liendane na matakwa ya sheria. Kimsingi, watunga sheria hawakuona haja ya kuweka upekee wowote kuwatenga wafungwa na sheria inayotaka watu wapime virusi vya Ukimwi kwa ridhaa yao na majibu yawe siri yao.”

Kwa upande mwingine, majaji hao walikataa maombi nane ya kina Msigwa ama kwa kutoungwa mkono na sheria yoyote au kwa waleta maombi kushindwa kutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yao.

Walisema vitendo binafsi ya ofisa magereza kukiuka sheria zinazoongoza namna ya kushughulika na wafungwa kama vile upekuzi wakiwa gerezani vinaweza kushughulikiwa kiutawala katika ngazi ya gereza husika.

Msigwa: Nilitembezwa uchi

Katika hati yake ya kiapo iliyotumika kama ushahidi katika maombi hayo, Msigwa ambaye Machi, 2020 alitiwa hatiani na kutakiwa kulipa Shilingi Milioni 40 au kwenda jela miezi mitano, alieleza kuwa alitembezwa mbele ya wafungwa wenzake akiwa uchi na alipekuliwa mwili wake wote sehemu za siri.

Alidai kuwa alilazimishwa kujisaidia kwenye ndoo ya chuma, maarufu gerezani au mahabusu kama ‘mtondoo’ iliyokuwa imetumiwa na wafungwa wengine, na kulazimishwa kupima virusi vya Ukimwi bila ridhaa yake na majibu yake kutolewa hadharani.

Msigwa alidai pia kuwa alilala kwenye chumba kilichokuwa na wafungwa wengi kuliko uwezo wake bila kuwa na vifaa vya kulalia huku wafungwa wengine wakilala sakafuni.

“Hapakuwa na chakula maalumu kwa wafungwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi, wanaougua shinikizo la damu na kisukari,” alidai.

Sugu: Nililazimishwa kujisaidia kwenye ‘Mtondoo’

Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama ‘Sugu’ alidai katika hati yake ya kiapo kuwa alipokuwa katika gereza la Ruanda, Mbeya baada ya kufungwa Februari, 2018 alilazimishwa kujisaidia katika mtondoo uliokuwa umetumiwa na wafungwa wengine bila kuoshwa.

“Utaratibu wa kutenga wafungwa ulikuwa bado unafanyika kama aina ya kuwaadhibu wafungwa wanaofanya makosa ambapo mfungwa anatengwa, anaachwa uchi na kuwekwa sehemu isiyo na mwanga bila vifaa vya kulalia. Wafungwa hawaruhusiwi pia kushiriki mazishi ya ndugu wa karibu kama wazazi, mke, mume au mtoto,” alidai.

Wanasheria hawajaridhika

Licha ya kupongeza uamuzi wa mahakama katika kipengele kilichohusu upimaji virusi vya Ukimwi bila ridhaa, wanasheria walioongea na Mwananchi, wameonyesha kutoridhishwa na mahakama kukataa maombi mengine ya waleta maombi.

Mwanasheria mkongwe na Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Rugemeleza Nshalla, alisema hauhesabu uamuzi huo kama ushindi dhidi ya sheria na utaratibu mbovu wa haki jinai nchini baada ya mahakama kukataa maombi mengine ya wanasiasa hao.

“Sijafurahishwa sana. Madai yaliyopelekwa yalikuwa yanatisha na usingetegemea mambo kama hayo yangetokea kwenye magereza yetu.

Tungetegemea magereza yetu yazingatie viwango vya kuthibitisha vilivyowekwa na kukubalika na vyombo vya kimataifa au vinavyotumiwa na nchi zilizostaarabika.

“Unataka ushahidi gani wakati mleta maombi amekueleza kwa kiapo kuwa ameyapitia yote anayoyalalamikia. Unadai ushahidi usiowezekana badala ya mahakama kushtushwa na hali hiyo na kutaka anayelalamikiwa alete ushahi kuonyesha hakufanya hayo?” alihoji

Kwa mujibu wa Nshalla, haikuwa sahihi kwa mahakama kutaka waleta maombi kupeleka ushahidi wa bila kuacha shaka katika kesi ya kikatiba kama ilivyo katika kesi za jinai,” alisema Nshalla akishauri waleta maombi waende Mahakama ya Rufaa.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresha wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe ameipongeza mahakama kwa uamuzi wake huku akiwataka walalamikaji kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa madai yao mengine.

“Unapokuwa mfungwa haimaanishi unapoteza haki zako kama binadamu wengine. Bahati mbaya mfumo wetu wa haki jinai na uendeshaji wa magereza unatokana na mfumo wa kikoloni. Uliwekwa mahususi kwa ajili ya kutweza utu wa mtu. Mfano kumpekua mtu akiwa uchi bila kujali utu au umri kulilengwa kumtweza,” alisema.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari