Habari, Utamaduni, Historia na Simulizi za Tanzania na Afrika Mashariki

Shirikisho lashauri Taekwondo Kufundishwa Katika Shule za Umma

3

Uongozi wa Shirikisho la mchezo wa Taekwondo Tanzania sasa wanataka elimu hiyo kuanza kufundishwa katika shule za umma zinazoendeshwa na serikali.

Tanzania Taekwondo Federation pia linashauri mchezo huo wa kundi la martial arts kuingizwa rasmi katika shughuli za michezo mashuleni na kuandaliwa mashindano maalum ya vijana.

“Tungependa mchezo wa Taekwondo uingizwe na kutambuliwa rasmi katika shule za msingi na sekondari za umma ili kuweza kusaidia kuinua na kukuza vijana kuanzia ngazi ya chini,” wanaongeza viongozi wa TTF.

Akizungumza jijini Arusha, Makamu Rais wa Shirikisho la Taekwondo Tanzania (TTF) Joseph Chuwa anasema kuwa Taekwondo inapaswa kufundishwa ipasavyo katika shule hizo za serikali.

Lengo ni ili kuweza kupata wachezaji ambao watafundishwa kuanzia ngazi ya chini kwaa ajili ya mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Anabainisha kwamba hivi karibu kulikuwa na mashindano ya Taekwondo ya vijana yaliyoandaliwa na shirikisho hilo  katika kumuenzi Baba wa taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Mashindano yalifanyika katika ukimbi wa Njiro complex, jijini Arusha lakini vijana wengi walioshiriki walitoka shule Binafsi, kuonesha kuwa taasisi za elimu za umma bado ziko nyuma katika sekta hii.

“Tunatoa wito kwa serikali waruhusu mchezo huu wa Taekwondo uingie katika shule za msingi na sekondari  ipasavyo ili kuibua vipaji,” aliomba Chuwa.

TTF pia inataka wazazi wapewe elimu juu ya mchezo huu kuwa ni mchezo ambao unazingatia nidhamu kwa ya hali ya juu.

Akizungumzia mashindano ya vijana yaliyofanyika alisema yalikuwa na ushindani mkubwa na hasa uelewa wa washiriki ulionekana kuwa wa kiwango cha juu.

Washiriki wa tamasha la Taekwondo ni kutoka visiwani Zanzibar, Mkoani Kilimanjaro, Jijini Dar-es-salaam, pamoja na vijana kutoka Arusha.

Mmoja wa wakufunzi wa mchezo wa Taekwondo, Ismail Abubakar kutoka Klabu ya Master Gym jijini Arusha, alisema bado ni changamoto katika kuwashawishi wazazi.

Anafafanua kuwa wazazi wengi wanaamini kuwa Taekwondo ni mchezo wa fujo, kupigana na pengine vijana wao wangeumia au kuwaumiza wenzao.

Lakini yeye anadai kuwa Taekwondo hasa ni mchezo unaosadia kujenga nidhamu kwa vijana.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari