Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Tani 40,000 za Mbolea zasambazwa kwa Wakulima wa Arusha, Manyara na Kilimanjaro

Tani zipatazo 40,000 zimesambazwa kwa wakulima wa mikoa mitatu ya Kanda ya Kaskazini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 katika harakati za kuboresha kilimo na usalama wa chakula nchini.

Shehena ya Mbolea yenye tani Zaidi ya 17,288 kati ya hizo imetolewa kwa wakulima walioko mkoani Arusha

Taarifa kutoka katika maonesho ya Kilimo, kuelekea sikukuu ya Nane Nane, kwa kanda ya Kaskazini, zinabainisha kuwa shehena nyingine za mbolea za uzito wa tani 18,557 zimesambazwa kwa wakulima katika mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, (TFRA), Godham Limpawe, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 pia tani zipatazo 2,840 za mbolea zilitolewa kwa wakulima wa mkoa wa Manyara.

Limpawe ameeleza kuwa Mamlaka hiyo imejizatiti vilivyo katika kuongeza kasi ya usambazaji wa Mbolea ili kuwafikia wakulima wote katika kanda ya Kaskazini kwenye msimu huu wa kilimo.

Meneja huyo amefafanua kuwa watafanya kazi kwa kushirikiana na vyama vya ushirika pamoja nakuongeza idadi ya vituo ili waingiza mbolea waweze kuwa na maeneo mengi ya ugawaji katika ngazi za wilaya

Maonesho ya 29 ya kilimo kuelekea Sikukuu ya Nanenane 2023 kwa kanda ya Kaskazini yanafanyika katika viwanja vya Nane-Nane, eneo la Njiro, kusini mwa jiji la Arusha, na yamezinduliwa rasmi na Spika wa Baraza la wawakilishi, Zanzibar Zuberi Ally Maulid.

Spika Maulid amesisitiza kuwa lengo kuu la maonesho hayo nikubainisha fursa zilizopo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini pamoja na kutoa elimu kwa ajili ya kuboresha shughuli zote za kilimo ikiwemo uzalishaji, usafirishaji na utafutaji masoko.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela, amesema Kilimo ni sekta muhimu nchini na kwamba maadhimisho ya mwaka huu yatumike kuwaunganisha wakulima wote kutoka mikoa yote na wale wa Visiwani Zanzibar.

Kitaifa, Maonesho ya Nane-Nane yanaadhimishwa mkoani Mbeya ambako kilele cha Sikukuu ya wakulima kama kawaida kitafikiwa siku ya Tarehe Nane, Mwezi wa Nane.

Kilimo ni sekta iliyoajiri takribani asilimia 80 ya wakazi wote wa Tanzania. Na ndiyo inayoongoza katika kuliletea taifa mapato ya fedha za kigeni yatokanayo na biashara ya kusafirisha na kuuza mazao ya chakula na biashara katika nchi za nje.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari