Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Tanzania kupeleka teknolojia ya mitambo ya kurutubisha nafaka nchini Benin

Tanzania inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutengeneza mitambo maalum ya kuongeza virutubisho kwenye nafaka na vyakula vingine, huku kukiwa na mpango wa kuipeleka teknolojia hiyo mpya nchini Benin.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mtambo wa kwanza jijini Arusha katika mkutano wa tisa wa wadau wa lishe unaofanyika jijini hapa.

“Hii ni hatua muhimu katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo nchini pamoja na kuondoa udumavu kwa watoto, masuala ambayo tayari Tanzania ilishapiga hatua kubwa katika utatuzi,” Waziri mkuu Majaliwa alisema.

Mtambo huo wa kurutubisha nafaka umetengenezwa kwa ushirikiano kati ya shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na taasisi ya teknolojia ya Dar-es-salaam (DIT) chini ya udhamini wa taasisi ya Global Alliance for Improved Nutrititon (GAIN).

Mashine hiyo maalum imezinduliwa rasmi na waziri mkuu Kasim Majaliwa katika kilele cha cha mkutano mkuu wa tisa wa wadau wa lishe hapa nchini,wenye kauli mbiu ya kuimarisha mifumo endelevu ya chakula kwa matokeo bora ya lishe na maendeleo ya rasilimali watu.

Kwa upande wake Paul Sangawe ambaye ni mkurugenzi Sera na Uratibu katika ofisi ya waziri mkuu amesema kuwa na mashine hiyo ya kuchanganya virutubisho, iliyoundwa nchini sasa inapatikana kwa gharama nafuu, ikilinganishwa na zile za awali zilizokuwa zikiagizwa kutoka nje.

Imeelezwa kuwa mashine kutoka nje zilikuwa zinagharimu shilingi Milioni 6 kwa moja, wakati hizi zinazoundwa nchini hununuliwa kwa gharama za shilingi Milioni 1.5 tu kwa moja.

Mkuu wa Programu katika taasisi ya GAIN, Dk Winfrida Mayilla amesema kuwa tayari mashine hamsini zimepelekwa katika mikoa ya Manyara, Kagera, Kilimanjaro, Tanga huku lengo likiwa ni kuzisambaza nchi nzima.

GAIN inafanya kazi katika nchi 11 barani Afrika na baada ya Tanzania, tuna mpango wa kupeleka teknolojia hii nchini Benin.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema kuwa kuna mpango wa kujenga kiwanda maalum kwa ajili ya kuzalisha mashine hizo kwa wingi, ili kuwezesha maeneo yote nchini kurutubisha nafaka na vyakula vingine.

Ameongeza kuwa bado utapiamlo ni changamoto kwani tatizo la udumavu nchini kwa sasa limefikia kiwango cha asilimia 30 na kwamba bado zinahitajika jitihada za kuutokomeza kabisa.