Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Wakala wa Misitu sasa kuweka mipaka kwenye maeneo yote yenye uoto wa asili nchini

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  imeanza kufanya utambuzi wa mipaka ya maeneo ya vijiji zenye uoto wa miti na hifadhi za misitu nchini, ili kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha yanasimamiwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya biashara ya hewa ya ukaa.

Mbali na hilo pia kutafanyika utambuzi wa aina ya mimea na wanyama waliomo ndani ya misitu hiyo ili kutengeneza thamani ya biashara hiyo itakayopelekea wamiliki na watunzaji kulipwa.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo katika ufungaji wa mradi wa miaka mitatu wa uhamasishaji wa utunzaji mazingira kwa vijana ujulikanao kama ‘sauti ya vijana’ iliyoratibiwa na shirika la world vision Tanzania katika Wilaya za Korogwe na Handeni Mkoani Tanga.

Prof. Silayo alisema kuwa kwa sasa serikali inatekeleza Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ambayo ni misitu inayonyonya hewa ukaa na kulipa wahusika hivyo wameanza utambuzi wa maeneo yenye misitu ikiwemo hifadhi Ili kujua kiasi kinachonyonywa na wamiliki na wahifadhi waweze kunufaika nayo.

“Utunzaji wa misitu sasa ina faida mbili kwetu, achilia mbali kiwango cha fedha ambacho nchi zilizoendelea zinalipa wahusika kwa ufyonzaji wa unit moja ya Caboni kulipwa hadi Dola 15, lakini pia inatengeneza hamasa mpya kwa nchi katika utunzaji wa mazingira na kuepuka athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi zinazopelekewa na shughuli za binadam” alisema na kuongeza…

“Niwapongeze sana shirika la world vision kwa mradi huu wa kuwahamasisha vijana juu ya utunzaji wa mazingira maana wao ndio watakaokuja kuwa waathirika wakubwa lakini zaidi niwahamasishe watanzania, mashirika na taasisi mbali mbali kuchangamkia biashara hii ya hewa ya ukaa kwa kupanda miti mingi zaidi na kuyatunza ili kunufaika na fedha zinazotolewa na nchi zilizoendelea”

Awali mkurugenzi wa shirika la world vision Tanzania James Anditi alisema mradi huo wa miaka mitatu wa uhamasishaji utunzaji mazingira kwa vijana ujulikanao kama ‘sauti ya vijana’ waliouratibu katika Wilaya mbili Mkoani Tanga ulifadhiliwa na umoja wa mataifa kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Alisema wamefanikiwa kupanda miti 101,700 ya matunda na vivuli katika vijiji 20 vya Wilaya za Korogwe na Handeni ambao zaidi ya vijana 1000 walihusika ikiwemo kupanda na kuihudumia iweze kustawi, lakini pia wamenufaika na Elimu mbali mbali za utunzaji wa mazingira, vyanzo vya maji lakini pia ujasiriamali kupitia misitu ikiwemo uwekezaji wa mizinga kwa ajili ya asali.

“Sisi tunahusika na watoto hivyo tuliona miti ya matunda ni muhimu pia kwa ajili ya lishe ya watoto na wanawake pia tukitambua wao ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabia ya nchi”. 

Nae mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Handeni, Saitoti Zelothe alisema kuwa mradi huo umesaidia sehemu kubwa ya malengo waliyowekewa na serikali ya Kila halmashauri kuhakikisha wanapanda miti milioni 1.5.

“Tumeshukuru sana maana imetusaidia kufikisha idadi ya miti tuliyopanda na kustawi kufikia 660,000 ambapo zingine tunatarajia kupanda msimu huu wa mvua za vuli kufikia malengo ya serikali ikiwa ni jitihada za kuhakikisha serikali inafikia malengo lakini pia kuokoa nchi kutokukumbwa na mabadiliko ya tabia ya nchi tena’

Nae Mmoja wa vijana walionufaika na mradi huo, Christina Dickson alisema kuwa mbali na kuisaidia jamii ya mkoa wa Tanga kunufaika na miti lakini pia wamepata Elim mbali mbali za kukwamua maisha yao kiuchumi ikiwemo uwekezaji salama na ujasiriamali.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari