Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Ukame Wateketeza Wanyamapori Ndani ya Hifadhi ya Burunge, Wilayani Babati

Twiga na Tembo wakijihifadhi chini ya miti kujikinga na jua kali kando ya bwawa linalokauka taratibu katika hifadhi ya Burunge

Ukame unaodaiwa kusababishwa na mabadiliko ya tabia nchi sasa umeanza kusababisha vifo kwa wanyamapori katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge.

Jumuiya hiyo iliyomo ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja wilayani Babati mkoani wa Manyara inapakana na hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara.

Burunge WMA ni jumuiya inayoundwa na vijiji 10 ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 24,319.

Licha ya wanyamapori kuathiriwa na ukame, maeneo ya mapito ya wanyamapori ya Kwakuchinja na Mswakini yamekumbwa na ongezeko la matukio ya ujangili.

Sambammba na hayo pia kumezuka migogoro baina ya wananchi na wanyamapori kutokana na wanyamapori hao kuanza kuingia maeneo ya vijiji kusaka maji na malisho.

Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise ameliambia Taifa Tanzania kuwa katika siku za karibuni wanyama wengi ndani ya ushoroba huo wamekuwa wakidindoka na kupoteza maisha kutokana na kukosa maji.

Wengine pia hufa kwa kunasa ndani ya matope mazito la vidimbiwini au mito inayokauka kutokana na ukame.

“Hali ni mbaya sana ya Ukame kutokana na mabadiliko ya tabia nchi tumeanza kupata kesi za wanyama kufa , wengine kuzama kwenye tope wakitafuta maji na wengine kuingia vijijini”alisema

Mwaise alisema,wanyamapori katika vijiji 10 ambavyo vinaunda jumuiya hiyo ya uhifadhi ambayo ipo kati kati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara, wameanza kuingiza kwenye nyumba za watu kunyang’anyana maji na watoto.

Alisema wanaomba Usaidizi wa wadau kukabiliana na changamoto ikiwepo kuchimba Maji .

Hata hivyo ili kukabiliana na hali hiyo , katika eneo la Kitalu Cha uwindaji kinachomikiwa  na Taasisi ya EBN kilichopo ndani ya Burunge WMA wameanza kuchimba mabwawa kusaidia maji kwa Wanyamapori.

Meneja Uhusiano wa EBN, Charles Sylvester alisema wameamua kuchimba mabwawa na kutoa maji kwa Wanyamapori ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani maji yamepungua sambamba na malisho.

“Hivi Sasa eneo letu kuna idadi kubwa ya Wanyamapori tofauti na miaka ya nyuma kabla ya kupewa Kitalu hiki ambapo pia Sasa Wanyamapori wamekuwa rafiki na watu na kuwezesha utalii wa picha na Makundi makubwa ya wanyamapori yamerejea katika Kitalu” alisema 

Alisema wameimarisha pia doria za kupambana na ujangili na uvamizi ndani ya hifadhi kwa kushirikiana na Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori (TAWA), askari wa Burunge WMA, Maafisa wanyamapori na askari wa hifadhi za Taifa (TANAPA).

” Tunatumia zaidi ya milioni 400 kwa mwaka kukabiliana na ujangili na hasa kipindi hiki Cha Ukame ambapo wanyamapori wanasogea vijijini”alisema 

Naye Mwenyekiti mstaafu wa Serikali ya Kijiji cha Vilima vitatu, Erasto Belela alisema athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa lakini Mahusiano mazuri baina ya vijiji na mwekezaji EBN imesaidia kupunguza athari.

“Uzalishaji chakula umepungua sana lakini kupitia Utalii walau vijana zaidi 120 wameajiriwa kwa mwekezaji ,tumesaidia kujengewa shule ,kupata maji na kupata mgao wa fedha za maendeleo”alisema.

Maeneo kadhaa nchini hasa mikoa ya Manyara na Arusha yameathirika na Ukame ambao unatokana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwepo mifugo kufa na watu kukosa maji na chakula.