Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Wanawake Milioni 1.6 nchini wanufaika kwa mikopo yenye thamani ya Bilioni 714 kutoka serikalini

Zaidi ya shilingi bilioni 714 zimetolewa kama mikopo kwa makundi maalum, wakiwemo wanawake wapatao milioni 1.6 nchini.

Waziri  Maendeleo ya Jamii jinsia, wanawake na makundi maalum Doroth Gwajima amesema kuwa mbali na mikopo hiyo, serikali inaendelea kufungua fursa nyingine kwa akina mama na vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.

Alikuwa akizungumza na wananchi katika maadhimisho ya siku ya mwanamke aishiye kijijini, yaliyofanyika wilayani Arumeru, Mkoani Arusha.

Waziri Gwajima aliwaasa wanawake kujenga tabia ya kutembelea taasisi za fedha zinazotoa mikopo na kuangalia fursa za kupata ile ambayo ni nafuu, isiyo na riba au yenye marejesho ya riba ndogo.

Pia amewasisitiza kina mama kuongeza thamani na kuboresha zaidi bidhaa zao na kufungua maduka mtandao ili kufanya biashara kidijitali na kuuza bidhaa zao hata nje ya mipaka ya nchi.

“Ingawa wanawake wa vijijini ndio wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara nchini lakinbi bado wanakabiliwa na changamoto kubwa za elimu, mitaji, mila na desturi kandamizi na mfumo dume unaowarudisha nyuma wengi wao,” alibainisha.

Mkuu wa wilaya ya Arumeru Emanuela Kaganda amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuadhimisha siku ya wanawake waishio vijijini kwa sababu hao ndio kiungo muhimu nchini katika uzalishaji wa chakula, malezi ya watoto, familia na hata uchumi.

Zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanaishi katika maeneo ya vijijini na wengi wao hujishughulisha zaidi na kilimo.

Siku ya mwanamke wa kijijini huadhimishwa kila mwaka ili  kutia hamasa kwa wanawake wa vijijini katika kuleta maendeleo na kuongeza uzalishaji.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Olevolosoi, Emanuel Lesion Ngailuva ameiomba serikali kuangazia suala la watoto wa kike kulazimishwa kuingia kwenye ndoa wakiwa bado wadogo na wenye kuhitaji kupata elimu.

Ameongeza kuwa mmomonyoko wa maadili umekuwa janga katika maeneo mengi vijijini hususan miongoni mwa vijana lakini kwa kukabiliana nalo wameanzisha mafunzo ya ufundi cherehani ambapo tayari eneo lao lina cherehani kumi ingawa nazo bado hazitoshi kwani uhitaji ni mkubwa.