Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Watu wasioona waomba kusaidiwa Bima za Afya

Jamii ya watu wenye ulemavu wa macho wameomba kusaidiwa kupata Bima Maalum ya Afya ili kuwasaidia katika masuala ya matibabu, na kupunguza utegemezi wao kwa watu wengine.

Mwenyekiti wa Chama cha wasioona (TLB) Mkoani Manyara, (Tanzania League of the Blind) Paulo Safari Akonaay anasema kuwa watu wengi wasioona wanaishi kama tegemezi kuanzia suala la kuoneshwa njia, chakula na malazi.

“Na utakuta watu tunaowategemea pia wana matatizo yao mbalimbali, hawawezi kutuhudumia kwa kila kitu,” alisema Akonaay, katika mkutano wa chama hicho uliofanyika wilayani Mbulu.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa TLB, mara nyingi watu wenye uoni hafifu na matatizo ya macho ndio hupata matatizo makubwa Zaidi katika changamoto za maisha na pia wao huwa vigumu Zaidi kupata kazi au kufanya biashara.

“Nadhani pia tungewezeshwa ruzuku katika umoja wetu, tungeweza kuanzisha shughuli za kufanya ili kupunguza au kujiondoa kabisa kwenye masuala ya utegemezi,” Akonaay aliongeza.

Chama cha Wasioona, pia kimetoa ombi kwa jamii na serikali kuwasaidia wanachama wake kwa fimbo za kutembelea, kwa ajili ya usalama barabarani, kutengwe maeneo ya kuvukia na pia kupewa vifaa vya elimu na hata mafunzo mbalimbali.

Imeelezwa pia kuwa walemavu wengi, hususan ambao hawana uwezo wa kuona, hawajajumuishwa kwenye mfuko maalum wa kuwasaidia watu wa kaya masikini ujulikanao kama TASAF.

Watu wasioona pia wanaomba kushirikishwa katika masuala mbalimbali ya jamii, vikiwemo vikao katika ngazi za kata na vijiji ili kuwaswezesha kupitisha malalamiko yao kwenye uongozi.

Afisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Tomic Simbeye ambaye pia ni mlezi wa chama hicho wilayani, amesema kwa sasa wanaendelea kutafuta wadau mbalimbali wa kuwasaidia watu hao kwa sababu serikali tayari ina majukumu mengi.

“Huwa pia kuna tamasha maalum la White Cane, au ‘Fimbo Nyeupe,’ ambalo hutumika kuwaleta wanachama pamoja na wadau wengine katika jukwaa moja kujadili changamoto zao,” alisema Simbeye.

Lakini kwa sababu matamasha haya hufanyika maeneo tofauti tofauti kumekuwa na tatizo la wengi kushnwa kuhdhuria kwa kutokana na gharama za safari.

Ameongeza kuwa watu wengi wasioona wengi hawana ajira, ni vigumu kupata mitaji na asilimia kubwa hawajasoma, pia huwa ni vigumu kampuni na taasisi kuwaajiri watu wasioona.

Simbeye anasema kuwa vifaa vya kuchapishia maandiko kwa watu wasioona pia ni tatizo kuvipata.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari