Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

‘Kwa nini waafrika wakitaka kwenda nchi nyingine barani humu lazima wapitie ulaya?’ Rais Samia ahoji

Mashirika ya Posta Barani Afrika yameshauriwa kutumia ndege za nchi wanachama katika kusafirisha vifurushi, mizigo na bidhaa zingine ili kuepuka gharama zinazotokana na matumizi ya mashirika ya ndege ya Ulaya, Asia na Marekani.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ushauri huo jijini Arusha katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Umoja wa Posta Barani Afrika, maarufu kama PAPU Tower, ambapo amesisitiza kuwa kuna kila sababu pia ya kuwezesha za mashirika ya ndege ya Afrika kufanya safari za moja kwa moja barani humu.

“Inasikitisha kuona kuwa kwa sasa ili mtu aweze kusafiri kwa ndege kutoka nchi moja ya Afrika kwenda nyingine, ni lazima kwanza apitie ama ulaya au marekani wakati hili ni bara moja na nchi zote ni majirani,” alisema.

Rais Samia pia alionesha masikitiko yake kwamba nchi 45 tu za Afrika ndizo zimejiunga na umoja wa posta barani humu wakati kuna nchi 55, n ahata baadhi ya nchi wanachama bado zinalegalega.

Awali katibu mkuu wa Umoja wa Posta Afrika, Dk. Sifundo Chief Moyo alilielezea jengo hilo refu Zaidi jijini Arusha kuwa kitakuwa ndio kitovu cha maendeleo ya kitekinolojia kwa huduma za posta barani Afrika.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na TEHAMA, Nape Nnauye alisema kuwa katika kuadhimisha uzinduzi wa kituo kipya cha mawasiliano ya posta barani Afrika, nchi kadhaa pia zimetengeneza stempu maalum za kumbukumbu ambazo zitapatikana katika mfumo wa kawaida na ule wa kidijitali.

Ujenzi wa makao makuu mapya ya Umoja wa Posta Barani Afrika uliotekelezwa kwa gharama za shilingi Bilioni 33, umefanikishwa kwa ubia kati ya PAPU na Serikali ya Tanzania.

Jengo hilo jipya lililopo eneo la Philips, katika kata ya Sekei, mkabala na barabara kuu ya Moshi-Arusha, litakuwa na ofisi mbambali za kitaifa na kimataifa, taasisi za fedha, migahawa na vituo maalum vya TEHAMA.

Wakati huo huo, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika, kutengeneza Ramani yake ya nchi kwa mfumo wa kidijitali.

Ramani hiyo iitwayo NaPA, ambayo sasa inashindana na ile ya Google, yaani Google Maps inawawezesha watumiaji kupata muongozo wa kuaminika wanapokuwa safarini nchi au pale wanapotafuta huduma za kijamii kama vile, benki, shule, hospitali, hoteli, au vituo vya mabasi.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Andrea Mathew, anasema kuwa ramani hiyo ya Tanzania, imejumuisha maeneo mengi, hususan yale ya vijijini ambayo mtu hawezi kuyakuta katika mfumo wa Google Maps.

Ramani ya NaPA inapatikana bure mitandaoni na pia hupakuliwa bure katika Google Play kwa watumiaji wa Android pamoja na Apple Store kwa wenye vifaa vya iOS.

“Ramani ya kidijitali ya NaPA pia inajumuisha anwani za makazi na maeneo mbali mbali,” alisema Naibu Waziri.

NaPA ingawa hasa ni mfumo wa kitaifa wa anwani na ramani Tanzania, lakini kwa kiasi kikubwa unaweza kupatikana na kufanya kazi vizuri hata katika nchi jirani.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari