Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Watumishi wa Umma walioachishwa kisa Vyeti, sasa kupata Shilingi Bilioni 32

MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF) unalazimika kulipa jumla ya shilingi Bilion 32 kwa watumishi wa umma 12,666 waliondolewa kazini kwa kile kilichodaiwa kuwa ni vyeti feki.

Mfuko huo wa PSSSF umefikia hatua hiyo baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia watumishi hao walipwe michango yao waliyokuwa wanachangia kwenye mifuko ya hifadhi walipokuwa kazini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, meneja wa uhusiano na Elimu kwa wanachama PSSSF, James Mlowe amesema kuwa hadi Sasa baada ya mchujo wa awamu ya kwanza zaidi ya watumishi 9,700 wameonekana kustahili kulipwa zaidi ya bilion 22.22.

“Mbali na hao wako zaidi ya watumishi 2800 ambao bado tunatengeneza madai yao ambapo yakikamilika wanapaswa kulipwa zaidi ya bilion 9.3 hivyo tunaomba ambao waliondolewa kazini Kwa sababu hii wajitokeze wajaze fomu na wafuate taratibu waweze kupata haki zao,” alisema Mlowe.

Mlowe alisema kuwa toka novemba mosi mwaka huu walipotakiwa kuanza mchakato wa ulipaji wamekwisha lipa jumla ya wadai 750 kati ya 9700 wanaopaswa kulipwa Kwa awamu ya kwanza, ambapo jumla ya bilion 22. 22 zimekwishatengwa Kwa ajili yao.

“Hao tayari hela zao zipo, tunawaita waje wajaze fomu na kufuata taratibu zote za madai ya mafao yao wachukue hizi hela na kama wamefariki basi warithi wajitokeze kupata haki hii”

Mlowe alisema kuwa kwa sasa wametengeneza mfumo mzuri wa kuhakikisha wanalipa mafao mapema ndani ya siku 30 tofauti na sheria inavyowataka ya siku 60 hii ni kutokana na maboresho makubwa waliyoyafanya ya kimfumo.

“Baada ya kuundwa kwa muunganiko huu miaka minne iliyopita tulipata changamoto ya kuchelewesha fedha za watu kutokana na deni kubwa tulilokuta la trillion 1.3 ambalo ilitulazimu kukaa na kutengeneza mfumo mzuri uliofanikisha malipo yote kukamilika” 

Amesema kuwa manufaa makubwa ya kuunganisha mifuko hii imepunguza gharama za uendeshaji kutoka bilion 128 hadi sasa ni bilion 67 pekee ambapo wameokoa zaidi ya bilion 46 

Awali Oktoba 26, 2022  Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako akizungumzia  uamuzi huo wa Rais Samia, alisema kuwa Watumishi hao ni wale walioondolewa katika utumishi wa umma katika shughuli maalum la uhakiki wa vyeti.

Zoezi hilo liliendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) katika kipindi cha kuanzia Oktoba 2016 hadi Aprili mwaka 2017.

Kufuatilia maelekezo hayo, mifuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF itarejesha michango ya wafanyakazi iliyowasilishwa kwenye mifuko hiyo bila kuhusisha michango ya mwajiri,” amesema.

Ndalichako alisema kuwa marejesho ya michango hiyo ilianza kufanyika kuanzia Novemba Mosi mwaka 2022, ambapo mtumishi husika anatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri wake akiwa na picha mbili za passport size.

Vingine anavyotakiwa kwenda navyo ni nakala ya taarifa za benki (Bank Statement) ya akaunti iliyo hai na nakala ya kitambulisho cha Taifa au mpiga kura au leseni ya udereva.

Alisema pia mtumishi atatakiwa kujaza hati ya ridhaa kwa aliyekuwa mwajiri wake.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari