Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Karatu Kujengewa Mnara wa Kumbukumbu ya Uhuru wa Tanganyika

Karatu ambayo ndio wilaya pekee nchini yenye mnara wa historia ya kuanzishwa kwa vijiji vya Ujamaa, sasa iko mbioni kujenga mnara mwingine wa kitaifa.

Baraza la wazee wilayani Karatu kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa pamoja wanajiandaa kujenga mnara wa kumbukumbu ya Uhuru wa Tanganyika, nchi ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanzania.

Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyojiri wakati wa mjadala wa kumbukumbu ya uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika katika mji wa Karatu mkoani Arusha.

Mdahalo uliandaliwa na serikali ya wilaya ya Karatu na ulijumuisha pia masuala ya maendeleo ya eneo hilo katika kipindi cha miaka 61 ya uhuru.

Mwenyekiti wa Baraza la wazee Charles Goranga alisema kuwa tayari wamekwisha kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa mnara huo.

Halmashauri imekusanya zaidi ya sh milioni Tano za kuanzia mradi huo wa kihistoria.

Mnara wa Uhuru mjini Karatu, pia utakuwa na sehemu ya Maktaba kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya waasisi wa Taifa pamoja na wazee waliokuwepo wakati wa harakati za kupambana na wakoloni.

Mgeni rasmi katika mdahalo huo alikuwa ni mkuu wa Wilaya ya Karatu Dadi Kolimba.

Kolimba aliwapongeza wakazi wa wilaya hiyo kwa harakati zao za kujiletea maendeleo.

Washiriki waliohudhuria majadiliano walijivunia  wilaya kupata maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali ndani ya  miaka 61 ya Uhuru, kutoka Tanganyika hadi Tanzania.

Walieleza mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa wilaya hiyo ambayo awali ilianza kama Tarafa na Sasa imekuwa moja ya wilaya saba, mkoani Arusha.

Karatu pia imefanikiwa kujenga hospitali ya wilaya inayohudumia watu takriban laki tatu.

Wilaya kwa sasa imeelezwa kuwa na shule zaidi ya 110 za msingi, hii ikiwa ni ongezeko la shule 101 kwani kabla ya Uhuru eneo hilo lote lilikuwa na shule 9 tu.

Karatu pia inajivunia shule 35 za sekondari. Kabla ya December 1961, wilaya ilikuwa na sekondari moja tu. 

Mdahalo huo ulitanguliwa na upandaji wa Miti katika maeneo ya hospitali ya wilaya ili kutunza mazingira, ambapo Miche zaidi ya 500 ilioteshwa.