Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Idadi ya Vifo vya Maporomoko ya Mlima Hanang yaendelea kuongezeka huku wengi wakidaiwa kupotea

Mamia ya watu wanadaiwa kuwa huenda wamefunikwa na tope zito, mawe miamba na miti wakati maporomoko kutoka Mlima Hananga yakiathiri vijiji Zaidi ya sita pamoja na Mji Mdogo wa Katesh, Mkoani Manyara, Kaskazini mwa Tanzania.

Hadi kufikia siku ya Jumatatu, Disemba 4, 2023 watu wapatao 50 walikuwa tayari wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa.

Hii yote ni kutokana na mafuriko na maporomoko makubwa ya udongo yaliyotokea katika miteremko ya kuuzunguka Mlima Hanang ambao ndio una kilele cha Tano kwa urefu nchini Tanzania, baada ya vile vya Mawenzi na Kibo juu ya Kilimanjaro, pamoja na Mlima Meru na Mlima Lolmalasin.

Maporomoko kutoka Mlima Hanang mkoani Manyara pia yameuathiri vibaya mji wa Katesh wilayani Hanang, pamoja na kusababisha kufungwa kwa barabara kuu inayoiunganisha mikoa ya Singida na Babati.

Waliojeruhiwa wamekuwa wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa hali zao zinapokuwa zimeimarika na wengine wamekuwa wakipelekwa hospitali kwa ajili ya kupata matibabu na kuondoka.

Taarifa zinasema kuporomoka kwa sehemu ya Mlima Hanang ndio chanzo cha mafuriko hayo. Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jumapili ya Tarehe 3 Disemba, imesababisha mafuriko ya tope zito katika eneo hilo.

Tarifa kutoka Manyara zinasema kuwa maporomoko kutoka Mlima Hanang yalisambaa eneo zima la upande wa kusini, kabla ya kufika katika mji mdogo wa Katesh ambao ndio Makao makuu ya wilaya hiyo.

Na upande ulioathirika Zaidi na maporomoko hayo makubwa ni ule ambako kuna vijiji kadhaa vikiwemo vile vya Gendani, Mogitu, Jorodom pamoja na Gedang’onyi.

Kina cha mtiririko wa tope hilo linakaririwa kufikia kimo cha wastani cha mtu mzima.

Maropomoko hayo yalibomoa nyumba kadhaa na kuzifunika nyingine nyingi. Pia yaliweza kusomba magari na vibanda vidogo vya mjini Katesh.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari