Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Mfanyabiashara wa Simiyu asombwa na Mafuriko akijaribu kuvuka daraja la Bumela na gari lake

Madhara ya mvua kubwa zinazonyeesha maeneo mbalimbalia nchiuni sasa yamefika mkoani Simiyu ambako mfanyabiahsra maarufu wa Bariadi amesombwa na maji wakati akijaribu kuvuka daraja lililofunikwa kwa maji.

Mfanyabiashara huyo aliyefahamika kwa jina la Gimbeshi Kalibangula mwenye umri wa miaka 32, aliyekuwa mkazi wa Nkololo wilayani Bariadi mkoani Simiyu amepoteza maisha kwa kusombwa maji ya mto Bumela uliopo wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Taarifa za awali zinasema kuwa Gimbeshi alikuwa akisafiri kutoka eneo la Mnada wa Langangabilili na alikuwa akiendesha gari lake binafsi kuelekea Nyumbani.

Inadaiwa kuwa gari hilo lilisombwa na maji ya mto uliofurika, wakati akivuka kwenye hilo daraja.

Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo wanadai kuwa waliona gari la Gimbeshi likisombwa na maji majira ya saa 11 jioni Desemba mosi.

Baada ya hapo, Mfanyabiashara huyo pamoja na gari lake walitoweka na juhudi za kuwatafuta hazikufanikiwa siku hiyo.

Hata hivyo, baada ya saa 48 ndipo mabaki ya gari la Gimbeshi yalipatikana kando ya mto, eneo la mbali zaidi kutoka darajani.

Gari lilikutwa maeneo ya wilaya ya Bariadi. Inadaiwa kuwa watu walijaribu kumuonya Gimbeshi asijaribu kuvuka darajani maana maji yalikuwa mengi lakini alikaidi.

Wakati huo huo, wananchi wa eneo la Nkjololo wameiomba serikali kujenga daraja jingine ambalo litakuwa juu zaidi ya hilo lililopo sasa ili wakati wa mvua kubwa, maji yasiweze kulifunika kama yafganyavyo kwenye daraja lililopo muda huu ambalo lipo chini kidogo.

“Kwa sasa eneo hilo ni hatari kwa binadamu na mifugo hasa kipindi hiki cha mvua, hivyo basi tunaiomba serikali itujengee daraja la juu au basi hili lililopo liinuliwe maana watu tunahangaika sana pake tunapokuwa safarini au wakati wa kwenda mnadani,” alilalamika Bi Happiness Joseph ,Mkazi wa Bumela.