Taifa Tanzania
Taifa Tanzania. Gazeti Huru la Afrika Mashariki linaloandaliwa kwa lugha ya kiswahili

Jinsi Mimea Vamizi inavyosababisha migogoro baina ya Binadamu na WanyamaPori

Mimea vamizi ambayo sasa inachipuka kwa wingi katika maeneo ya hifadhi, inadaiwa kuwa kwa sasa ndio chanzo kikubwa cha migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara maalum ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walipotembelea Jumuiya ya Hifadhi ya wanyamapori ya Burunge, iliyoko wilayani Babati, mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Katibu wa Jumuiya hiyo, Benson Mwaise, mimea vamizi inayoota katika sehemu za hifadhi huathiri maeneo ya malisho hivyo kulazimisha wanyama kuhama kutoka sehemu iliyotingwa na majani hayo mageni na kwenda kutafuta maeneo mengine ya kujipatia chakula.

Na mara nyingi wanyama hao wakiwa katika harakati za kutafuta maeneo mengine yenye majani mazuri hujikuta wameingia katika mashamba au makazi ya watu, hivyo kusababisha tafrani kubwa.

“Hivi sasa tunashirikiana na watafiti kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, ili kubaini upana wa tatizo pamoja na ukubwa wa maeneo yaliyoathirika,” alisema Mwaise na kuongeza kuwa hiyo ni pamoja na kutafuta njia sahihi za kukabiliana na mimea hiyo vamizi katika hifadhi.

Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA), iliyoanzishwa kupitia muungano wa vijiji kumi, impo katikati ya mapito au ushoroba wa wanyamapori ujulikanao kama Kwakuchinja.

Makao Makuu ya Jumuiya ya Hifadhi ya Burunge (JUHIBU)

Kwakuchinja (Corridor) ni mapito ya asili ya wanyamapori yanayounganisha hifadhi mbili za taifa za Tarangire na Ziwa Manyara, pamoja na shamba kuu la Manyara Ranch, zote hizo zikiwa katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Ushoroba wa Kwakuchinja hapo awali ulikuwa na ukubwa wa Kilometa za Mraba 600 ila sehemu kubwa kwa sasa imevamiwa na shughuli za kibinadamu.

Eneo hilo la uhifadhi wa kijamii pia limepakana na maziwa mawili ya Burunge na Manyara ambayo kwa asilimia kubwa hutegema maji ya mto mkubwa wa Tarangire.

Hivi karibuni waandishi wa Habari walitembelea eneo hilo la hifadhi ikiwa ni sehemu ya mafunzo maalum ya mazingira na hifadhi ya Bioanuwai yanayoendeshwa na Taasisi ya Nukta Afrika, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), kupitia mradi wake wa ‘Tuhifadhi Maliasili!’

Hifadhi ya Burunge (WMA) ambayo imo ndani ya ushoroba wa Kwakuchinja, yenyewe ina ukubwa wa kilometa za mraba 283 na imepakana na eneo la Mswakini Chini.

Burunge ni hifadhi ya kijamii inayoundwa na vijiji kumi, vikiwemo Magara, Mwada, Sangaiwe, Ngolley, Vilima Vitatu, Kakoi, Minjingu, Olasiti, Maweni na Manyara.

Vijiji hivyo kumi vyote vimo ndani ya kata tatu za Mwada, Magara na Nkaiti, wilayani Babati.

Na wataalamu wanakiri kuwa eneo hilo muhimu kwa hifadhi ya mazingira, mapito ya wanyama pamoja na shughuli za kitalii, limeathirika sana na uoto wa mimea migeni vamizi inayotishia afya za wanyamapori pamoja na wale wa kufuga.

Huku wataalam wakiendelea kuumiza vichwa kutafuta suluhu ya tatizo kubwa la mimea vamizi nchini, wahifadhi wanaonya kuwa linaweza kusababisha wanyamapori kuhama kabisa kutoka maeneo yao ya asili.

Mimea vamizi pia imeathiri kwa kiasi kikubwa eneo la Malisho katika hifadhi ya Taifa ya Arusha (ANAPA) ambako awali, kamishna msaidizi wa uhifadhi, Yustina Kiwango alibainisha kuwa Zaidi ya asilimia 17 ya hifadhi hiyo imefunikwa na magugu hayo.

“Mimea vamizi, yakiwemo ‘matufaa ya sodoma,’ marufu kama Ndulele, imeoteana ndani ya eneo lenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 55,” alisema Kiwango na kuongeza kuwa Hifadhi ya Taifa ya Arusha (National Park), ina ukubwa wa Kilometa za Mraba 332.

Pamoja na kufunika kabisa maeneo ya malisho ya wanyamapori, mimea vamizi pia imetengeneza vichaka vya miiba ambavyo vimekuwa vikifunga maeneo ya mapito ya wanyama na kusababisha baadhi ya viumbe hao kuhamia nje ya hifadhi na hata kwenye makazi ya watu.

Sehemu nyingine iliyoathirika na mimea vamizi ni eneo la hifadhi jumuishi ya Ngorongoro (NCA) ambako pia magugu mengine mageni yaliyopewa jina la ‘Makutiani,’ yamechipuka katika sehemu mbalimbali ikiwemo ndani ya bonde maarufu yaani Kreta.