Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Siku Moto Ulipolipuka kwenye jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar-es-salaam

Ilikuwa saa za asubuhi ya tarehe 5 Julai mwaka 1984.

Wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliamka kwa mshangao baada ya kusikia na kuliona moshi mkubwa na mzito ukiwa umetanda eneo zima la jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kifupi kasma kuu ya nchi ilikuwa inaungua kwa moto uliokuwa umesambaza moshi mkubwa na mzito juu ya anga la mji eneo la ufukweni mwa Bahari ya Hindi.

Tukio hilo lilitokea kiasi cha miaka zaidi ya 40 iliyopita, kipindi cha serikali ya awamu ya kwanza ya utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kama kawaida, Watanzania wakiwemo waliokuwa na kazi na ambao hawakuwa na cha kufanya, walifurika maeneo jirani ya jengo hilo ambalo ndilo hasa Kasma ya Nchi ili kushuhudia likiwaka moto.

Ni kipindi ambacho hapakuwa na televisheni, redio binafsi wala simu za mikononi kwa hiyo tukio kama hili ilibidi watu watoke maeneo mbalimbali ya jiji kwenda kuangalia, kushangaa na kutunga hadithi za kwenda kusimulia nyumbani baadae.

Magari kibao ya zimamoto na wafanyakazi  jeshi la uokozi wakihangaika kuudhibiti.

Vile vile vikosi vya majeshi ya usalama vilikuwa yamefurika eneo hilo ili kuhakikisha hapatokei purukushani, vurugu au matukio ya uporaji wakati wa kupambana na janga hilo la moto mkubwa.

Kwa ufahamisho tu ni kwamba jengo lililoungua ni lile la awali, au asili au ‘orijino’.

Yaani jengo la mwanzo kabisa la benki hiyo lililofunguliwa Julai, 1969 na Mwalimu Julius Nyerere.

Ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa zipatazo sita  – wakati huo –  uligharimu shilingi milioni kumi na moja (11), ambazo zilikuwa ni sawa na Dola za Kimarekani milioni 1.6.

Kwa mahesabu ya sasa, si rahisi kuamini kwamba jengo kubwa kama hilo liligharimu kiasi kidogo cha pesa kama hicho!  Hata hivyo, ikumbukwe kwamba jengo hilo lilifunguliwa miaka Zaidi ya hamsini iliyopita.

Hata hivyo, jengo hilo ambalo liliungua sehemu zote ‘laini’ na kubaki likiwa zima katika sehemu zote ‘ngumu’ kama vile kuta, zege na vyuma na kadhalika, lilikarabatiwa na kuanza kutumika, japokuwa lilifanyiwa mabadiliko kadhaa kwa ndani na nje.

Habari kamili au za wazi kuhusu chanzo cha moto huo na hasara zake, hazikutolewa kwa wazi sana licha ya ujio wapelelezi kutoka Uingereza ambao waliwasili nchini kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kutoa ripoti kwa mamlaka husika. 

Hata hivyo, ni dhahiri hati na kumbukumbu mbalimbali ziliteketea katika moto huo ambapo shughuli nyingi zilikuwa zinafanyika kwenye ‘makaratasi’.

Tofauti na taswira ya wakati huo, makao makuu ya benki hiyo hivi sasa yamebadilika sana, kwani jengo hilo lililoungua hivi sasa liko katikati ya majengo pacha marefu, kila moja likiwa na ghorofa 20, ambayo yalikamilika kujengwa mwaka 2006. 

Matokeo yake, majengo hayo mawili, kaskazini na kusini mwa jengo la awali yamelifanya hilo jingo la zamani kuonekana kama ‘mbilikimo’ katikati ya majitu makubwa.

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari