Habari, Makala na Simulizi kutoka Afrika

Vijiji Kumi Meatu Kupimwa ili kuepusha migogoro kati ya binadamu na wanyamapori

Vijiji kumi ambavyo vinaiunda Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Makao, wilayani Meatu, vinatarajia kupimwa upya kwa ajili ya maandalizi ya mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Zoezi hilo linalenga kubainisha na hatimaye kugawa maeneo ya hifadhi ili kuyatenganisha na shughuli nyingine za kijamii, katika kuleta suluhisho la migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.

Kwa mujibu wa viongozi wa eneo husika, Mpango huo wa matumizi bora ya ardhi, unatarajiwa kusaidia kupunguza hali ya sintofahamu baina ya shughuli za uhifadhi na shughuli nyingine tofauti za kiuchumi zinazotekelezwa na wakazi wa eneo hilo.

Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Makao (WMA) ya wilayani Meatu, mkoani Bariadi, imo katika eneo ambalo linapakana na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori Tengefu la Maswa.

Akizungumza na mwananchi Katibu wa Makao WMA, Jeremiah Bishoni anafafanua kuwa tayari mchakato umeanza kuvisaidia vijiji hivyo kupimwa  ili kuwezesha kutenga maeneo mbali mbali kulingana na mahitaji.

“Tunatarajia vijiji vikipimwa vyote, itasaidia kuwezesha mpango wa kupitia eneo zima la Hifadhi ya Jumuiya na kufanikisha mpango wa usimamizi wa ardhi ya WMA,” aliongeza.

Alisema Makao WMA katika kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii  inatarajiwa kuwa na vikao tarehe 8 Februari 2023 na wawekezaji katika eneo hilo na tarehe 9 Februari 9 wanatarajiwa kukutana na wajumbe wa baraza la WMA wa AA na mwekezaji katika eneo hilo.

Afisa Wanyamapori wilayani Meatu, Deusdedit Martin  akizungumzia mikakati ya kuboresha shughuli za uhifadhi na Utalii, katika wilaya hiyo, alisema wamepanga  kuvitembelea vijiji vyote vilivyopo ndani ya WMA  na baadae kuwa na vikao na wadau wa uhifadhi na Utalii.

Martin pia amegusia suala la ongezeko la idadi ya Tembo katika maeneo hayo.

Afisa wanyamapori huyo amekiri kuwa Tembo wamekuwa wakiingia katika maeneo ya makazi ya watu na kuzua tafrani pamoja na changamoto zingine nyingi.

Amesema kuwa tayari halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wameanza kutoa elimu kwa wakazi wa Meatu kuhusu mbinu rafiki za kuzuia Tembo kufika katika maeneo yao na kuharibu mashamba..

“Hii ni baada ya kugundua kuwa kuna watu  walikuwa wakiwafukuzia wanyama hao kuelekea kwenye makazi ya watu alimradi tu wazue tafrani.” Alifafanua

Habari Zingine

Maoni yamefungwa, lakini 0naweza kushea habari